Social Icons

Facebook Twitter LinkedIn Google+

April 06, 2015

FILIKUNJOMBE AIMWAGIA SIFA TUME YA TAIFA YA UCHAGUZI

Deo Filikunjombe akiongea na waumini wa kanisa la Anglikana Mavanga



 Filikunjombe akipokea zawadi kutoka kwa bibi mmoja wa Mavanga

 Filikunjombe pamoja na familia yake akipata maelezo toka kwa Padre Faraja Mapunda wa kanisa la Anglikana la Mavanga ambapo alichangia bati 300 zinazotosha kuezeka kanisa hilo



MBUNGE wa jimbo la Ludewa Mh.Deo Filikunjombe ameipongeza tume ya taifa ya uchaguzi kwa kitendo cha kusogeza mbele mchakato wa upigaji kura wa katiba inayopendekezwa hivyo amewataka wananchi wilayani Ludewa kujitokeza kwa wingi kujiandikisha katika daftari ya kudumu ya wapiga kura.

Filikunjombe aliyasema hayo jana katika ibada ya maazimisho ya sikukuu ya Pasaka katika kanisa la Anglikana kata ya Mavanga wilayani hapa alisema kwa kufanya hivyo tume ya Taifa ya uchaguzi inastaili pongezi kwani kulikuwa na maswali mengi kutoka kwa wananchi yasiyo na majibu hivyo majibu yamepatikana.

Alisema kuwa hakuna haja ya kufanya haraka mchakato huo wa katiba mpya kwani wananchi bado hawajapewa muda wa kutosha wa kuipitia katiba hiyo hivyo kwa kipindi hiki ni muda muafaka sasa kwa wananchi kutumia muda mwingi kuielewa katiba yao ambayo itafanya kazi miaka mingi ijayo.

Filikunjombe alisema kuwa aliyeanzisha mchakato wa katiba mpya ambaye ni Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania alikuwa na maono ya mbali na nchi yake kwani ni rais ambaye atakumbukwa na watanzania kwa mengi mazuri likiwemo la kukubali kubadirisha katiba kwa maana hiyo katiba hiyo itakuwa ni mali ya wananchi kama utasomwa na kueleweka ili kupitishwa.

“Naipongeza tume kwa kusogeza mbele tarehe ya upigaji kura kuhusiana na katiba inayopendekezwa lakini hasa nampongeza rais Dkt Jakaya Mrisho Kikwete kwani ni rais ambaye atakumbukwa na wananchi kwa dhamira yake ya dhati ya kuanzisha mchakato huu wa katiba hakika ni rais ambaye anaipenda Tanzania na ndio maana hana haraka hata waswahili wanasema mambo mazuri hayahitaji haraka”,alisema Filikunjombe.

Kuhusiana na kauli za Maaskofu kuipigia kura ya hapana katiba pendekezi Filikunjombe  alisema Serikali inatakiwa kutoa elimu ya kutosha kwa viongozi wa dini upende wa wakristo na waislamu kuhusu Mahakama ya Kadhi kwani jambo hilo lisiwagawe watanzania kutokana na itikadi za kidini wala kisiasa.

Alisema kunasoleza malumbalo katika suala hilo ni kutokuwa na elimu ya kutosha kuhusiana na jambo lenyewe hivyo kuanzia wananchi,madiwani hata wabunge wanatakiwa kupata elimu ya kutosha ndipo muafaka upatikane lipi la kulifanya na lipi la  kuliacha.

Katika maazimisho ya sikukuu ya Pasaka Filikunjombe alitoa msaada wa vifaa vya ujenzi katika shule ya chekechea ya kanisa Katoriki parokia ya Mavanga bati miamoja geji 28,saruji mifuko 150 na rangi pia ujenzi wa kanisa la Anglikana la Mavanga bati 300 ili kukamilisha ujenzi wa kanisa hilo ambalo limekaa muda mrefu bila kuezekwa kutokana na kukosekana kwa fedha ya kununulia bati.

Filikunjombe aliwasihi waumini wa makanisa hayo kuliombea Taifa liweze kudumisha amani hasa kipindi hiki kigumu kwani taifa lipo katika mchakato wa mambo mengi likiwemo suala la uchaguzi mkuu Oktoba  mwaka huu,pia aliwataka kuandaa viongozi waadirifu katika mchaguzi mkuu ili kulijenga taifa katika misingi ya amani na utulivu ambayo imezoeleka.

Naye Diwani wa kata ya Mavanga Mh.Edwin Mgaya kwa kupitia chama cha Mapinduzi alimshukuru Filikunjombe kwa utaratibu wake aliyojiwekea wa kusheherekea sikukuu zote na wananchi wake kwa kutembelea kata na vijiji kwani kwa kufanya hivyo ameweza kupata fulsa nzuri ya kuongea na wananchi na kujua changamoto zinazo wakabili.

Mh.Mgaya alisema wananchi wamekuwa na imani kubwa na mbunge wao pamoja na chama chake cha CCM kwani mengi anayoyafanya yanaonekana hivyo wananchi wamekuwa mstari wa mbele kumsikiliza na kuyatendea kazi yale wanayoelezwa na Filikunjombe kwani ni mbunge pekee aliyefanya kazi na wananchi hadi vijijini kwa kuwatembelea mara kwa mara na kuwatia moyo.

Mwisho.

No comments: