RAIS WA ZAMBIA AFARIKI DUNIA.
Hayati, Michael Sata aliyekuwa rais wa Zambia |
Habari na Salim Kikeke wa BBC,
Serikali ya Zambia imesema Rais wa nchi hiyo Michael Sata
amefariki dunia wakati akiendelea kupatiwa matibabu kwa maradhi ambayo
hayakutajwa.
Rais Sata, 77, alifariki katika hospitali ya King Edward VII
jijini London, Uingereza Jumanne usiku.
Vyombo vya habari vimesema alifariki baada ya "mapigo
ya moyo kwenda kasi ghafla".
Haijafahamika mara moja nani atachukua nafasi yake ya urais.
Suala hilo huenda likajadiliwa na baraza la mawaziri la Zambia litakalokutana
Jumatano asubuhi.
"Kwa moyo mzito natangaza kifo cha rais wetu
mpendwa," imesema taarifa ya waziri Roland Msiska iliyosomwa kwenye TV ya
taifa.
"Nawaomba muwe watulivu, muungane kwa amani katika
kipindi hiki kigumu," ameongeza kusema Bwana Msiska.
Mapema mwezi huu taarifa nchini Zambia zilisema Rais Sata
alikuwa amekwenda nje ya nchi kwa matibabu, huku kukiwa na tetesi kuwa alikuwa
taabani.
Baada ya kuondoka nchini humo, waziri wa ulinzi Edgar Lungu
alitajwa kukaimu urais.
Makamu wa rais Guy Scott mara nyingi hukaimu urais. Hata
hivyo ana asili ya Scotland na wazazi wake hawakuzaliwa Zambia, hivyo hatoweza
kuchukua urais kutokana na vipengele ndani ya katiba.
Akijulikana kama "King Cobra" kutokana na matamshi yake makali, Bwana Sata alichaguliwa kuwa rais wa Zambia mwaka 2011.
No comments:
Post a Comment