Mabadiliko ya wakuu wa mikoa nchini
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete amefanya uteuzi wa wakuu wapya wanne wa Mikoa, amewahamisha wengine sita na ameamua kuwa wengine watatu watapangiwa kazi nyingine.
Taarifa iliyotolewa mjini Dodoma jioni ya leo, Jumatano, Novemba 5, 2014 na Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue inasema kuwa, Wakuu wapya wa Mikoa ni Bi. Halima Omari Dendego ambaye anakuwa Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Dkt. Ibrahim Hamisi Msengi ambaye anakuwa Mkuu wa Mkoa wa Katavi, Bi. Amina Juma Masenza ambaye anakuwa Mkuu wa Mkoa wa Iringa na Bwana John Vianney Mongella ambaye anakuwa Mkuu wa Mkoa wa Kagera.
Taarifa inasema kuwa kabla ya uteuzi wake Bi. Dendego alikuwa Mkuu wa Wilaya ya Tanga, Dkt. Msengi alikuwa Mkuu wa Wilaya ya Moshi, Bi. Masenza alikuwa Mkuu wa Wilaya ya Ilemela na Bwana Mongella alikuwa Mkuu wa Wilaya ya Arusha.
Taarifa hiyo inasema kuwa Wakuu hao wapya wa Mikoa wataapishwa kesho, Alhamisi, Novemba 6, 2014 saa saba mchana, Ikulu, Dar es Salaam.
Aidha, taarifa hiyo imesema kuwa Wakuu wa Mikoa ambao watapangiwa kazi nyingine ni Kanali (Mst) Fabian Massawe wa Kagera, Dkt. Christine Ishengoma wa Iringa na Kanali Joseph Simbakalia wa Mtwara.
Wakuu wa Mikoa ambao wamehamishwa vituo vya kazi ni Bwana Magesa S. Mulongo ambaye anakwenda Mkoa wa Mwanza kutoka Arusha, Dkt. Rehema Nchimbi ambaye anakwenda Mkoa wa Njombe kutoka Dodoma, Bwana Ludovick John Mwananzila anakwenda Tabora kutoka Lindi, Kepteni (Mst) Anseri Msangi anayekwenda Mkoa wa Mara kutoka Njombe na Mhandisi Everist Ndikilo ambaye anakwenda Arusha kutoka Mwanza.
Wengine waliohamishwa ni Luteni (Mst) Chiku A.S. Galawa ambaye anakuwa Mkuu wa Mkoa wa Dodoma kutoka Tanga, Dkt. Rajab Rutengwe ambaye anakwenda Mkoa wa Tanga kutoka Katavi, Bi Fatma Mwasa ambaye anakuwa Mkuu wa Mkoa wa Geita kutoka Tabora na Bwana Magalula S. Magalula ambaye anahamishiwa Lindi kutoka Geita.
Taarifa hiyo imesema kuwa Wakuu wa Mikoa ya Dar es Salaam, Kigoma, Kilimanjaro, Manyara, Mbeya,Morogoro, Pwani, Rukwa, Shinyanga, Ruvuma, Singida na Simiyu watabakia kwenye vituo vyao vya sasa.
Aidha, Rais Kikwete amefanya uteuzi wa Wakuu wapya wa Wilaya, kuhamisha baadhi yao na kutengua uteuzi wa baadhi.
Taarifa kamili itatolewa na Waziri Mkuu baada ya kuwa wamepangiwa vituo vya kazi.
Imetolewa na;
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu – Dar es Salaam.
05 Novemba,2014
No comments:
Post a Comment