Social Icons

Facebook Twitter LinkedIn Google+

October 09, 2014

VURUGU ZA WANAFUNZI ZAIFUNGA SHULE YA SEKONDARI YA NJOSS KWA MWEZI MMOJA.

 Moja ya majengo yaliyoweza kuchomwa moto na wanafunzi usiku wa kuamkia octoba 8 mwaka huu
 Baadhi ya vifaa vya wanafunzi vilivyotolewa nje mara baada ya kuanza kuungua kwa bweni namba nane.
 watu kazini
mwandishi wa habari wa kituo cha Uplands Fm cha Njombe Bw. Michael Ngilangwa  akiendelea kushuhudia tukio hilo.

Na James Festo, Njombe.

SERIKALI Mkoani Njombe imeifunga shule ya sekondari ya Njombe kufuatia vurugu iliyojitokeza usiku wa kuamkia octoba 8, ambapo katika vurugu hizo wanafunzi hao wamefanikiwa kuchoma bweni la wanafunzi, karakana na kuharibu mali mbalimbali za shule na walimu na kisha kwenda kuharibu majengo ya shule ya msingi Kilimani kwa mawe iliyopo karibu na shule hiyo.

Akizungumza katika shule hiyo  kwa niaba ya kamishna wa Elimu ,Ofisa elimu Elimu Mkoani hapa Said Kinyaga Nyasiro, aliamuru kufungwa kwa shule hilo hadi  novemba nane mwaka huu  kutokana na wanafunzi wa shule hiyo kukosa nidhamu hadi kufikia hatua ya kuchoma bweni lenye uwezo wa kuchukua wanafunzi 102.

Nyasiro alisema kuwa shule hiyo imefungwa kwa mwezi mmoja na pindi itakapofulimiwa kila mwanafunzi atatakiwa kufika shuleni akiwa na shilingi laki moja na nusu ikiwa na ulipaji wa uharibifu lilotokea katika shule hiyo  wenye thamani ya shilingi milioni 101.


Kutokana na tukio hilo jeshi la polisi lililazimika kutumia mabomu ya machozi ambapo kwa mujibu wa askari waliokuwepo katika eneo hilo walisema kuwa hali ingekuwa mbaya zaidi kama polisi wasingewahi kwani mbali na kuchoma bweni na karakana walianza kuvamia nyumba za walimu na kuharibu mali zao, kwani walichoma pia gari la mwalimu wa taaluma ambaye jina lake halikufahamika na kisha kuvunja duka lake na kuharibu vitu mbalimbali kabla ya kuvamia nyumba vya Mkuu wa shule Bernard Wliiam na kuvunja vioo vya madirisha.

 Mwalimu Bernard William Mkuu wa shule hiyo alisema bweni hilo limeteketea kabisa pamoja na vitanda vya shule na mali za wanafunzi vikiwemo vitabu, wakati ambapo wakiwa wanaendelea na ukarabati wa bweni jingine lililoungua moto hivi karibuni.

Alisema chanzo cha wanafunzi kufikia uamzi huo ni kudai kuonewa kwa wenzao 30 waliosimamishwa masomo kutokana na utovu wa nidhamu, ambapo 29 kati ya hao wanakabiliwa na kosa la kutoroka shule na kwenda kufanya fujo disko katika chuo cha maendeleo Njombe wakati wa sherehe za kuagwa mkuu wa chuo hicho aliyestaafu, huku mmoja akisimamishwa kutokana na kukamatwa na simu darasani wakati sheria za shule haziruhusu.



"madai wanayolalamikia hayana msingi wowote, wenzao walitoroka na kwenda disko chuo cha maendeleo ya jamii Njombe na kufanya fujo, mmoja wao alijeruhiwa vibaya mguu mpaka sasa anatembelea magongo  tumewasimamisha wanadai ni uonevu" alisema Mwalimu huyo.

 Maria Mdete ni Mwenyekiti wa bodi ya shule hiyo alisema linasikitisha sana, hasa ikizingatiwa kwamba wanafunzi wanaowatetea hawajafukuzwa shule bali walisimamishwa tu, na kwamba juzi Oktoba 7, mwaka huu walikutana na wazazi wa wanafunzi hao na kuwaeleza makosa ya watoto wao na kuwaambia watawajulisha kwa barua lini warudi shule.

" kila mwanafunzi tulikuwa tunamwita na mzazi wake na kuzungumza nao, na tuliazimia kila mzazi atajulishwa kwa barua lini watarudi shule na wala hatukufikia uamzi wa kuwafukuza. Sasa nashangaa jana (juzi) usiku wamechoma bweni, karakana na kuharibu mali mbalimbali za shule na kuchoma gari la mwalimu na kuharibu duka lake, kwa kweli wameitia hasara kubwa sana shule hii," alisema Mdete.

Kamanda wa polisi mkoa wa Njombe, Fulgence Ngonyani pia alifika katika eneo la tukio na kujionea uharifu uliofanywa na wanafunzi hao na kufanya kikao cha ndani na mkuu wa shule hiyo, na mara bada ya mkutano huo  alithibitisha kutokea kwa tukio hilo, na kusema kuwa atalizungumzia zaidi mara baada ya kufanya tathmini  ili kubaini thamani ya mali zilizoteketea.

Mpaka majira ya saa 7 mchana polisi walikuwa wakiendelea kuwasomba wanafunzi  kwenye magari kwenda kituo cha polisi kwa mahojiano.

Mkuu wa wilaya ya Njombe Sarah Dumba alifika shuleni hapo na kuzungumza na wanafunzi, ambapo alitoa wito kwa wanafunzi kuacha utovu wa nidhamu pindi wanapokuwa shule badala yake wazingatie kazi iliyowapeleka ya kusoma.

Alisema tukio hilo ni limesababisha hasara kubwa kwa serikali ambapo sasa itaanza kuingia gharama upya za kukarabati majengo yaliyoharibiwa badala ya kufanya shughuli nyingine za maendeleo na kwamba pia linawatia hofu walimu.

Tukio hilo linakuja ikiwa mwaka mmoja tu tangu bweni jingine la shule hiyo liteketee kwa moto ambalo kwa sasa liko kwenye hatua za mwisho kukarabatiwa
>>END.

No comments: