Social Icons

Facebook Twitter LinkedIn Google+

October 26, 2014

KATIBU MKUU WA WIZARA YA KILIMO NA CHAKULA AWATIA MOYO WAKULIMA WA MAHINDI LUDEWA

 Katibu mkuu wizara ya kilimo na chakula Bi.Sophia Kaduma akiongea na uongozi wa kijiji hivi karibuni Ludewa kijijini







KATIBU mkuu wa wizara ya kilimo na chakula Bi.Sophia Kaduma amewatia moyo wakulima wa mahindi wilayani Ludewa katika Mkoa wa Njombe kwa kuwataka kutokukata tamaa ya kuendeleza kilimo hicho kwani Serikali kila mwaka itatenga bajeti yae kununua mahindi ya wakulima hao.

Kauli hiyo ya Bi.Kaduma imekuja baada ya wakulima wilayani hapa kukata tamaa ya kuendeleza kilimo cha mahindi kwa msimu ujao kutokana na kutoridhishwa na ununuzi unaoendelea kufanywa na Serikali kwa mwaka huu kwani mpaka sasa wakulima wamekua wakiilalamikia Serikali kushindwa kununua mahindi yao licha ya kupewa mbolea za ruzuku na kuitikia kaulimbiu ya kilimo kwanza.

Akitoa malalamiko ya kushindwa kuuza mahindi yake mbele za katibu mkuu wa wizara ya kilimo na chakula aliyefanya ziara yake hivi karibuni katika wilaya ya Ludewa ili kuona mwenendo wa ununuzi wa mahindi unaofanywa na Serikali mkulima mmoja aliyejitambulisha kwa jina la Daudi Luoga mkazi wa kijiji cha Amani alisema mpaka sasa anagunia 3500 lakini hazijanunuliwa.

Bw.Luoga alisema alitumia fedha nyingi shambani ili kujikwamua kiuchumi akishirikiana na mkulima mwenzie aliyemtambulisha kwa jina la Asanje Luoga lakini juhudi za kuiuzia Serikali mahindi yao zimegonga mwamba kwani mpaka sasa mahindi yanayonunuliwa ni ya wakulima wadogo wenye roba chini ya 50 hali ambayo ni hatari kwa wakulima wenye mahindi mengi na wasio na uwezo wa kuyasafirisha kwenda nchi jirani.

“Tunashangazwa na kauli za viongozi wanaotembelea katika vituo vya ununuzi maana kila wakifika kauli yao ni moja ya kuwazuia wapimaji wasipime kwa mkulima ambaye ana mahindi mengi,kauli hiyo imeleta utata na kutujengea uadui na wenye mahindi machache kwani wanapotuona tu hutukunjia yuso na tunaonekana kama si watanzania tena wenye haki ya kuthaminiwa kama wapigakura wengine”,Alisema Bw.Daudi.

Alisema Serikali inapaswa kutambua kuwa wakulima wa hali ya kati kama yeye ndio wanaoweza kuwasaidia wakulima wadogo vijijini pale wanapopatwa na matatizo kwa kuwapa mikopo ya mbolea hivyo aliiomba Serikali kutambua mchaango wao katika jamii kwa kuyanunua mahindi yao na si kuwatenga na kuwakatisha tamaa ya kuendelea kulima tena wakati hawana uwezo wa kuyasafirisha nje ya nchi kama wakulima wakubwa.

Katibu  mkuu wa kilimo na chakula Bi.Kaduma akijibu malalamiko hayo alisema Serikali inawajari wakulima wote hivyo wasikate tamaa ya kuendelea kulima mahindi kwani kwa mtu mwenye uwezo wa kuyasafirisha kwenda nchi jirani aende ofisi ya mkuu wa mkoa atapewa kibari bira masharti ili aweze kuyauza kwa urahisi.

Bi.Kaduma alisema ni ukweli usiopingika kuwa kwa mwaka huu mahindi yamezalishwa kwa uwingi nchi nzima hivyo Serikali haiwezi kuyanunua yote inachokifanya ni kuyanunua kwa wakulima wadogo ambao hawana uwezo wa kuyasafirisha kwenda kuyauza kwingine lakini wenye roba zaidi ya 600 hao wanauwezo mkubwa wa kuyasafirisha na kuyauza kwingine.

Aliwapongeza wakulima nchini kwa kuitikia sera ya kilimo kwanza kwa kuzalisha kwa wingi hivyo aliwataka kuwa makini na walanguzi ambao wanatoka nchi jirani kwani tayari inasadikika walanguzi kutoka nchini Kenya wameanza kununua mahindi kwa bei ya kutupwa wilani Ludewa katika maeneo ya kijiji cha Amani ambako kuna uzalishaji mkubwa wa zao la mahindi katika mkoa wa Njombe.

Mwisho.

No comments: