Social Icons

Facebook Twitter LinkedIn Google+

September 30, 2014

RC NJOMBE AWATAKA WAKULIMA KUUZA MAHINDI MASAFI



Bw.Nyangasa akiangalia shughuri za ununuzi wa mahindi

          Diwani wa kata ya Ludewa Monica Mchilo akiongea na wanahabari

Mkuu wa Mkoa wa Njombe Kapten mstaafu Aseri Msangi amewataka wakulima mkoani hapa kuwa na utamaduni wa kusafisha mahindi yao na kuyatunza kwa uangarifu kabla ya kuyauza kwa wakala wa hifadhi ya chakula ya Taifa.
Kapten Msangi aliyasema hayo jana wakati wa ziara yake ya kikazi katika vituo vya ununuzi wa mahindi wilayani Ludewa ambako wakala wa hifadhi ya chakula Taifa(NFRA)wananunua mahindi ya wakulima.
Alisema ifike wakati wakulima wawe na utamaduni wa kuuza mahindi masafi kwani Serikali inapata hasara kubwa kwa kununua mahindi machafu na yasiyo na viwango ambayo yatakataliwa katika soko la kimataifa na nchi jirani.
Aliwataka wasimamizi wa manunuzi kuangalia zaidi wakulima wa hali ya chini ambao wametumia mitaji yao yote katika kilimo kwani yasiponunuliwa mahindi yao hali ya kiuchumi itazidi kuwa mbaya zaidi tofauti na wale wakulima wakubwa ambao wanaweza kuyasafirisha mahindi hayo hadi nchi jirani.
“nawaomba ninyi mliopewa dhamana na Serikali ya kuyanunua mahindi haya myanunue yakiwa masafi na yenye ubora ili yauzike kimataifa pia hawa wakulima wadogo ndio wanaotakiwa kuanza kuyauza mahindi yao kwenu na si hawa wenye roba zaidi ya 600 kutokana na ukweli usiopingika kuwa hawa wengine wanauwezo wa kuyasafirisha lakini hawa wadogo hawana uwezo huo’’,Alisema Kapten Msangi.
Kapten Msangi aliyasema hayo kutokana na uzalishaji mkubwa wa mahindi nchini kwa mwaka huu tofauti na kiwango cha ununuzi wa mahindi hayo kilichopangwa na Serikali hivyo bila kuwasaidia wakulia wadogo basi wimbi la umaskini litakuwa kubwa nchini.
Aidha meneja wa hifadhi ya chakula ya Taifa(NFRA) kanda ya nyanda za juu kusini kituo cha Makambako(NFRA)Bw.Abdilla Nyangasa alisema Serikali imetoa fedha za kununulia mahindi kwa wakulima na kuacha mambo mengine hivyo wasimamizi wa vituo vya ununuzi wanapaswa kuzitendea haki fedha hizo kwa kununua mahindi yenye ubora.
Bw.Nyangasa alisema kinachotakiwa kwa wakulima ni kuleta mahindi masafi ili yaweze kuuzika katika mataifa mengine yenye shida ya chakula kwani baadhi ya wakulima wamekuwa wanatabia ya kuuza mahindi machafu wakiamini NFRA watafanya kazi ya kuyasafisha hali ambayo si sahihi.
Alisema wakulima wakitanzania wanapaswa kuanza kujifunza namna ya kuhifadhi chakula ambacho kitaweza kuuzika katika mataifa mengine na si kuishi kwa mazoea kwakufanya hivyo wakulima wanaweza kujiingizia fedha nyingi za kigeni na kuachana na umaskini uliokithiri.
Bw.Nyangasa alisema hata sita kumfukuza kazi mfanyakazi yeyote wa NFRA  ambaye itathibitika kuwa aliruhusu kupima mahindi machafu kwa kupewa rushwa na mkulima mkubwa kwani kwa kufanya hivyo atakuwa amekiuka misingi ya kazi aliyopewa kuifanya na Serikali.
Alisema katika kanda ya Makambako ni tani elfu arobaini tu ndizo zilizopangwa kununuliwa na Serikali hivyo wasimamizi wa manunuzi wanatakiwa kuwa makini kutokana na hali halisi ya uzalishaji mkubwa wa mahindi kwa mwaka huu hali hii inaweza kusababisha mianya ya rushwa kwa wanaotaka kutangulia kupima mapema mahindi yao.
 Bw.Nyangasa aliwaomba wakulima kushirikiana na viongozi wa wilaya katika kufichua mambo yote ambayo si sahihi yanayofanywa na wasimamizi wa manunuzi katika vituo na kutoa taarifa mapema katika vyombo husika pale wanapoona kuna harufu ya rushwa.
Mwisho.

No comments: