Social Icons

Facebook Twitter LinkedIn Google+

June 02, 2014

DC LUDEWA AWATAKA WANANCHI KUJITOKEZA KATIKA MAPOKEZI YA MWENGE WA UHURU.


                              Mkuu wa wilaya ya Ludewa Bw.Juma Solomon Madaha

Mkuu wa wilaya ya Ludewa katika mkoa wa Njombe  Bw.Juma Solomon Madaha amewataka wananchi wa wilaya yake kujitokeza kwa wingi katika mapokezi ya mbio za Mwenge wa Uhuru unaotarajiwa kukimbizwa wilayani humo Julai 2 mwaka huu.

Bw.Madaha aliyasema hayo leo katika kikao cha maandalizi ya mapokezi ya Mwenge wa uhuru kilichofanyika katika ukumbi wa Halmashauri ya wilaya Ludewa ambacho kiliwakutanisha wadau  mbalimbali wakiwemo waandishi wa habari.

Akitoa ratiba ya mbio za mwenge wa uhuru katika wilaya ya Ludewa alisema Mwemge huo unatarajiwa kupokelewa katika kijiji cha madope Julai 2 mwaka huu asubuho saa 2.00 na kukimbizwa katika kata na vijiji vilivyoko pembezoni mwa barabara kuu kuelekea Manda.

Alizitaja kata zitakazopitiwa na Mwenge wa Uhuru ni pamoja na kata za Madope, Mlangali,Mawengi,Luana na Ludewa kata nyingine ni Nkomang'ombe,Luilo,Masasi,Manda na Ruhuhu,pia alisema Mwenge huo unatarajia kulala katika kata ya Manda.

"Nawaomba wananchi wote bila kujali itikadi za vyama vyenu mjitokeze kuupokea mwenge wetu wa Uhuru ambao tutaupokea wilaya ya Njombe na kupita nao barabara kuu ambapo tunatarajia kulala Manda na tutaukabidhi Julai 3 mwaka huu katika kijiji cha Lituhi wilayani Nyasa katika Mkoa wa Ruvuma",alisema Bw.Madaha.

Aidha alibainisha kuwa Mwenge wa uhuru utafungua miradi mbalimbali ya maendeleo hivyo wananchi wote wafike maeneo ambayo miradi itafunguliwa ili kusikia taarifa mbalimbali za miradi hiyo ambayo itasomwa na viongozi wao wa vijiji.

Bw.Madaha aliwataka wananchi wa eneo ambalo utafanyika mkesha wa Mwenge wa Uhuru kuepuka michepuko na kubaki njia kuu kwani bila kufanya hivyo kunaweza kusababisha kasi ya maambukizi ya virus vya ukimwi kuongezeka kutokana na baadhi ya watu wasio waaminifu kutumia mikesha kama hiyo kwaajili ya mambo ya anasa.

 Mwisho.

No comments: