Social Icons

Facebook Twitter LinkedIn Google+

May 24, 2014

WANANCHI WA KATA YA MKONGOBAKI WAFANYA HARAMBEE NA KUKUSANYA SHILINGI LAKI TANO.

Diwani wa kata ya Mkongobaki Mh.Ally Mtweve akitoa maendelezo kwa mwenyekiti wa halmashauri khusiana na mradi wa maji 
 Mh.Ally Mtweve akitolea maelezo kuhusiana na ujenzi wa barabara ya Ugera
 Mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya ya Ludewa Mh.Kongo akiongea na wananchi wa Ugera

Akinamama akichota maji katika tanki lililojenga na shirika la PADECO

Viongozi wakikagua ofisi ya Kata ya Mkongobaki
Tanki lililojengwa na shirika la PADECO
 Mh.Kongo akihesabu fedha zilizopatikana katika harambee
                   hii ni barabara ya Ugera

Jumla ya shilingi laki tano zimepatikana katika harambee iliyofanyika hivi karibuni ili kuharakisha ujenzi wa ofisi ya kata ya Mkongobaki na kufanikisha maendeleo shule za msingi katika kata hiyo iliyoko kijiji cha Ugera wilayani Ludewa katika mkoa wa Njombe.

Akiendesha harambee hiyo mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya ya Ludewa Mh.Mathei Kongo alisema ili kufanikisha maendeleo ya vijiji na kata ni lazima wananchi wajitambue katika kutoa michango yao ya hali na mali pasipo kuitegemea Serikali.

Mh.Kongo alisifu maendeleo ya kata hiyo kwa kuwa na barabara inayopitika na kuwepo uhakika wa maji safi na salama ambapo baadhi ya vijiji wilayani humo bado havina huduma kama hizo.

Nachukua fulsa hii kuwasifuni wananchi wa kata ya Mkongobaki,viongozi wa kata,vijiji pamoja na Diwani wenu kwa maendelo mliyoyafanya kwani ni mfano wa kuigwa tofauti na kata hata vijiji vingine ambavyo bado vinasubiri mkono wa Serikali katika kuleta maendeleo”,alisema Mh.Kongo.

Akisoma taarifa ya maendeleo Diwani wa kata ya Mkongobaki Mh.Ally Mtweve alisema licha ya kuwa wananchi wa kata hiyo wanafanya kazi kwa juhudi ili kujiletea maendeleo pia Halmashauri ya wilaya ya Ludewa imekuwa ikitoa fedha za miradi katika kata hiyo.

Mh.Mtweve alisema katika ujenzi wa ofisi ya kata ambao unafanyika katika kijiji cha Ugera ambako ndiko makao makuu ya kata ya Mkongobaki Halmashauri imetoa kiasi cha shilingi 15 milioni na wananchi wamechangia shilingi 2 milion jumla ya fedha zote zilizoanza ujenzi ni shilingi 17 milioni lakini bado hazijaweza kumaliza ujenzi wa jengo hilo.

Alisema kata hiyo imekuwa na miradi mitatu mikubwa ambapo mradi wa barabara umegharimu kiasi cha shilingi 36 milioni,mradi wa ujenzi wa ofisi ya kata shilingi 17 milioni na mradi wa maji ambao umejengwa na shilika lisilo la kiserikali umetumia kiasi cha shilingi 102 milioni.

Mh.Mtweve alisema mpaka sasa wananchi wa kata hiyo wanaendelea kujitolea katika kazi mbalimbali ili kuhakikisha maendeleo ya kata hiyo ambayo ni mpya inakwenda sawa na kata kongwe kama zile za Lugarawa na Mlangali.

Alimshukuru mbunge wa jimbo la Ludewa Mh.Deo Filikunjombe kwa kuwa mstari wa mbele katika maendeleo ya kata hiyo kwani wakati mwingi amekuwa akiwatembelea na kutoa ushauri katika mambpo mbalimbali yakimaendeleo.


Mh.Mtweve aliwataka wananchi wa kata ya Mkongobaki kuacha ushabiki wa vyama badala yake kujikita katika maendeleo bila kujali itikadi za vyama kwani katika maendeleo hakuna chama cha siasa.

Aidha mkurugenzi wa shirika lisilo la kiserikali la PADECO Bw.Wilbard Mwinuka ambalo linafanya usambazaji wa maji katika kijiji cha ugera kata ya Mkongobaki na kitongoji cha Muhumbi katika kijiji cha Lipangala alisema mradi huo unatarajia kukamilika ifikapoJuni mwaka huu.

Bw.Mwinuka alisema shirika la PADECO lenye makao yake makuu mkoani Njombe kwa kushirikiana na Halmashauri ya wilaya ya Ludewa limeweza kupata ufadhiri nchini Hispania kiasi cha shilingi 102 milioni ambazo zinafanya kazi ya ujenzi wa matenki na utandikaji wa bomba.

Alisema mpaka sasa tayari kazi hiyo iko ukingoni kwani imeweza kufanyika haraka kutokana na uelewa mkubwa wa wananchi wa vijiji husika ambao walifanya kazi kwa kujitolea ili kuharakisha miradi ya vijiji vyao.

Alizitaja changamoto alizokumbana nazo ni pamoja na upatikanaji wa mchanga wa kujengea matanki ya maji,usafirishaji wa vifaa vya ujenzi kwani msimu wa mvua barabara ziliharibiwa sana hivyo usafirishaji wa vifaa kutoka Njombe ulikuwa ni shida.

Aidha aliisifu Halmashauri ya wilaya ya Ludewa kwa kutoa ushirikiano kwa mashirika yasiyo ya kiserikali pale yanapopata miradi ya maendeleo hivyo amezitaka halmashauri nyingine kuiga mfano huo katika kuharakisha maendeleo kwa wananchi.

Mwisho.

No comments: