Social Icons

Facebook Twitter LinkedIn Google+

May 02, 2014

MAZISHI YA BABA MAZAZI WA MBUNGE FILIKUNJOMBE KUFANYIKA SIKU YA JUMANNE LUDEWA MJINI ,VIONGOZI MBALI MBALI WAKIONGOZWA NA RAIS KIKWETE WATUMA SALAM ZA RAMBI RAMBI




Marehemu.Mzee Frolian Filikunjombe kulia akisalimiana na katibu mkuu wa CCM Bw.Kinana alipotembelea wilaya ya Ludewa.

BABA mzazi wa mbunge wa  jimbo la Ludewa Deo Filikunjombe mzee Frolian Filikunjombe (78) amefariki dunia akiwa katika ndege angani akitokea nchini Dubai katika matibabu .

Huku  viongozi  mbali mbali akiwemo Rais wa Jamhuri ya muungano wa Tanzania Dr Jakaya Kikwete ,waziri mkuu Mizengo Pinda,waziri wa Wizara ya Wanawake, Jinsia na Watoto Sophia Simba na waziri mkuu mstaafu Edward Lowassa wakituma salam za rambi rambi kwa mbunge Filikunjombe kwa msiba   huo mzito.
Akizungumza na mwandishi wa habari hizi juu ya msiba  huo mbunge Filikunjombe ambae alikuwa jimboni katika kikao cha Halmashauri kuu ya CCM wilaya na kuhani msiba wa mzee maarufu katika  kijiji cha Shauri Moyo mzee John Mtitu baba wa msanii wa bongo Movi  Wiliam Mtitu alisema  kuwa taarifa ya  kifo hicho ameipata jana majira ya jioni kutoka kwa mdogo  wake Philip Filikunjombe aliyekuwa naye  huko.
Mbunge Filikunjombe alisema kuwa mzazi wake huyo alikuwa akisimbuliwa na ugonjwa wa kansa, kwanza kwenye kibofu cha mkojo na baadaye kwenye uti wake wa mgongo na kupelekwa kwa mara ya kwanza nchini India kwa matibabu .


"Kule India walimwanzishia dozi ya mionzi.na  alikuwa anakuja nyumbani kuendelea na chemotherapy.....
wakiwa kwenye ndege angani kutoka Dubai kuja Dar es Salaam  mzee alilalamika kusikia baridi....
Philip - mdogo wetu - aliyekuwa naye kumsaidia akamnyooshea kiti ili kiwe kama kitanda na akamfunika blanketi. ....akalala usingizi hakuamka tena "

Akielezea  taratibu za mazishi  alisema  kuwa mazishi  yamepangwa kufanyika siku ya jumanne wiki ijayo katika mji wa Ludewa na kuwa baba  askofu wa kanisa la RC Njombe Alfred Leonhard Maluma ndie ataongoza ibada ya mazishi  hayo.

Hata  hivyo  alisema  kuwa  wanaLudewa  waliopo  jijini Dar es Salaam, jamaa na marafiki wote  wataaga mwili  huo siku ya kesho  jumamosi kabla ya  kuanza  safari ya  kuelekea  Ludewa kwa mazishi safari itakayoanza siku hiyo ya jumamosi.

Pia  amewashukuru madaktari  wote  wakiwemo wa hapa nchini ambao  walipata  kumhudumia  wale wa India na Dubai kwa jitihada zao za kunusuru maisha ya mzazi  wake ambae alimpenda sana japo  Mungu kampenda  zaidi .

Amewashukuru  wananchi  wa jimbo la Ludewa ambao  muda  wote  walikuwa  karibu kwa kuulizia maendeleo ya afya  yake  pamoja na kumuombea apone kwani alisema ni juzi tu alipofika kuhani msiba wa mzee Mtitu pale Shauri Moyo na  kuzungumza na waombolezaji ambao walianza kufanya maombi ya kumwombea mzee Filikunjombe .

Aidha  aliwashukuru viongozi mbali mbali  wakiongozwa na Rais Kikwete kwa  kumfariji kwa kumtumia salam za rambi rambi mara tu walipopokea taarifa ya msiba  huo.

Kamanda  wa UVCCM mkoa wa Iringa  Salim Abri Asas ,mbunge wa  jimbo la Isimani Wiliam Lukuvi na mbunge wa viti maalum mkoa  wa Iringa Ritta Kabati wameeleza  kusikitishwa na kifo  hicho cha mzee Filikunjombe na  kumpa  pole mbunge  Filikunjombe na kumwombea  kwa Mungu ampe roho ya uvumilivu wakati  huu wa maombolezo.

Mungu ailaze roho ya marehemu Frolian Haule Filikunjombe mahala pema peponi Amina.

No comments: