Social Icons

Facebook Twitter LinkedIn Google+

April 08, 2014

MAMLAKA YA MAJI TUKUYU YAPANDA MITI 146 KWENYE VYANZO VYA MAJI.

MAMLAKA ya maji Tukuyu (TUWASA) wilayani Rungwe mkoani Mbeya imepanda miche ya miti 146 katika vyanzo  viwili vya maji vilivyopo kata ya kawetele ili kulinda mmomonyoka wa udongo katika vyanzo hivyo pamoja na kuazimisha siku ya upandaji miti duniani itakayofanyika mwishoni mwa mwezi huu.

Akizungumza mara baada ya zoezi hilo la upandaji miti kukamilika mwenyekiti wa malaka hiyo wilayani Rungwe Anosisye Mwasege akiwa na timu ya viongozi 13 waandamizi wa malaka hiyo alisema kuwa wameamua kuendesha zoezi hilo la upandaji miti lililoenda sambamba na utoaji wa semina jinsi ya utunzaji wa mazingira kwa wakazi wanaoishi karibu na maeneo ya vyanzo hivyo.

Alisema kuwa katika chanzo cha Mwakasege wamepanda miti 104,chanzo cha hodi wamepanda miti 42,na kufikia idadi hiyo ya miti 146 na kwamba aliwashukuru wananchi kwa kukubali kushiriki zoezi hili pamoja na kuwa walitembea umbali mrefu  kutoka katika makazi yao hadi kwenye vyanzo hivyo.

Mwasege aliongeza kuwa mkakati wa mamlaka hiyo ni kupanda miti inayohifadhi mmomonyoko wa udongo katika vyanzo vyote vya maji vilivyopo wilayani humo ili kulinda,kuhifadhi na kutunza mazingira katika maeneo hayo na kuwa siku ya maji duniani kiwilaya yatafanyika katika kata hiyo.

Mwenyekiti wa Kitongoji cha kawetele chini Syemu Melele mbali na kupongeza zoezi hilo pia aliwataka wananchi wa kitongoji chake wanaoishi karibu na vyanzo hivyo kuwa walinzi na kuwafichua wale wote watakao onekana kutaka kuharibu  vyanzo na kufanya uchafuzi wa mazingira katika maeneo hayo.

Afisa mtendaji wa Kata hiyo Nickolaus Kosama aliwataka wana nchi kufuata maelekezo ya maafisa hao na kuyafanyia kazi ili kuleta tija katika maboresho wanayoyafanya juu ya utunzaji wa mazingira pamoja na kulinda mmomonyoko wa udongo katika vyanzo hivyo na kuwa atawashughurikia wale wote watakao kutwa na hatia ya kufanya uharibifu katika vyanzo hivyo.

Anyimike Mwasakilali diwani wa kata hiyo na mwenyekiti wa Nccr Mageuzi wilayani Rungwe aliwatoa hofu maafisa wa mamlaka hiyo juu ya usalama katika vyanzo hivyo na kusema kuwa wananchi wa kata yake ni wasikivu hivyo watavilinda vyanzo hivyo na kuheshimu maagizo na ushauri uliotolewa na wataalam na y eye atahakikisha mambo yanaenda vizuri kama yalivyokusudiwa.

Wananchi waliohudhuria na kushiriki zoezi hilo wameupongeza uongozi wa mamlaka hiyo kwa hatua waliyoifanya pamoja na elimu waliyopatia juu ya utunzaji wa mazingira pamoja na kutunza vyanzo hivyo na kwamba wao wenyewe ndiyo wakakuwa walinzi wa vyanzo hivyo na kuwa watatoa taarifa kwenye serikali ya kijiji iwapo wataona kuna mtu amefanya uharibifu ili ashughurikiwe.
MWISHO.

 Na Ibrahim Yassin,Rungwe


No comments: