Filikunjombe akiwa amebebwa na wananchi wake wilayani Ludewa
Waananchi wakimsikiliza Filikunjombe katika moja ya mikutano yake wilayani Ludewa.
MBUNGE wa Jimbo la Ludewa (CCM), Deo Filikunjombe amewataka wananchi wa Ludewa kutoa ushirikiano wakutosha kwa wafanyakazi wa Tanesco ambao hivi punde watakwenda katika baadhi ya vijiji wilayani Ludewa ili kupima maeneo ambayo yatapitiwa na nguzo za umeme kwaajili ya kusogeza huduma ya umeme kwa wananchi walioko vijijini.
“Changamoto kubwa katika miradi mingi ya umeme ni kutokana na wananchi kuwa wagumu zaidi katika kujitolea maeneo ambayo nguzo za umeme zinapita na kutaka kulipwa fidia kwa kila kitu... tunaona katika baadhi ya maeneo hapa nchini wananchi wanataka kulipwa fidia kwa kila kitu hata kama ni mihogo watu wanataka kulipwa,“ alisema Filikunjombe ambaye aliwaasa wana Ludewa tuwe tayari kupokea mradi huu wa umeme ambao utafungua milango ya uchumi Ludewa.
Akiishukuru REA kwa kukubali kupeleka huduma ya umeme vijijini kwa wananchi wake, Filikunjombe amevitaja vijiji 14 ambavyo vitapelekewa umeme kuwa ni vijiji vya:Ludewa kijijini kitongoji cha Ngalawale, Kimerembe, Nkomang’ombe, Luilo, Lifua, Kipangala, Masasi, Lihagule, Igalu, Mbongo, Nsungu, Ilela, Ngerenge na Kipingu.
Nishati hiyo ya umeme ambayo inayotarajia kwenda katika vijiji 14 ambavyo vipo katika tarafa ya Masasi itaanzia katika mitambo ya umeme ya Shirika la TANESCO Ludewa mjini na kuelekea katika vijiji hivyo.
Filikunjombe ametoa kauli hizo kwa nyakati tofauti hivi karibuni
wakati wa ziara yake ya kuzungumza na wajumbe wa serikali za vijiji
vitakavyonufaika na mradi huo wa umeme vijijini ambao utatekelezwa kwa
mpango wa pamoja kati ya REA na shirika la ugavi wa umeme nchini
(TANESCO) ambao utaanza hivi karibuni. “Lengo la serikali iliyopo
madarakani chini ya Rais Jakaya Kikwete,“ alisema Filikunjombe “Ni
kuona wananchi wanatatuliwa changamoto mbali mbali zinazowakabili,
ikiwemo ya nishati ya umeme vijijini.“
Alisema iwapo wananchi wanaozunguka maeneo ya mradi huo wa umeme watakubali kuonyesha ushirikiano wao kwa TANESCO upo uwezekano wa mradi huo kuanza mapema. Amewataka wananchi kuangalia uwezekano wa kusamehe baadhi ya miti ya maembe, mikorosho na mihogo itakayong‘olewa kwa ajili ya kupisha nguzo na nyaya za umeme.
Filikunjombe amevitaja vijiji vingine vitakavyopelekewa umeme kuwa ni vijiji vya Kilondo, Luwana, Mholo, Mavanga, Mbugani, Mundindi, Shaurimoyo, Lugarawa, Mkiu, Kiyombo, Mlangali, Milo, Mavala, Mapogoro, Ludende, Madindo, Mkongobaki, Amani, Nindi, Ntumbati na Lupingu.
“Ninajivunia kuwa na mwakilishi makini anayetutetea na kutupigania vyema sisi wananchi wake,“ alisema Stanley Kolimba (63) ambaye kwa sasa ni mwenyekiti wa CCM wilaya ya Ludewa.
Kolimba alisema juhudi anazozifanya Filikunjombe za kuwaondoa gizani wananchi wa vijijini ni nuru ya matumaini katika jimbo hilo kwani toka nchi ipate uhuru wake mwaka 1961 vijiji hivyo havijawahi kuona mwanga wa umeme.
“Hiki ndicho tunachohitaji wananchi. Tunataka kuona mbunge tuliyemchagua anafanya yale ambayo sisi tumemtuma kule bungeni,” alisema Edwin Haule(Spika) Diwani wa Kata ya Ruhuhu, iliyoko pembezoni mwa ziwa Nyasa.
“Ludewa tumewahi kuwa na wabunge wengi. Lakini kiukweli hatujawahi kuwa na mbunge mchapa kazi kama Filikunjombe ambaye kimsingi utendaji wake unatufanya wananchi tuzidi kuwa na imani ya kuendelea kuongozwa na mbunge huyu. Na kama inawezekana - kwa utendaji huu wa mbunge wetu - tungependekeza Filikunjombe awe mbunge wa maisha,” alisema Haule.
Toka amechaguliwa mwaka 2010, Filikunjombe amefanya mambo mengi makubwa kwa ajili ya wananchi wake; barabara za Ludewa kuanza kuboreshwa kwa kiwango cha lami, uchimbaji wa madini ya makaa ya mawe na chuma miradi ambayo yote imeanza utekelezaji katika kipindi chake; na hivyo kuwafanya wananchi wa Ludewa nao waanze kunufaika na matunda ya uhuru.
Mwisho.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment