Yohana Nkwera akiwa hana miguu
Mmkazi wa Ludewa kijijini kanda ya juu wilayani Ludewa, Mkoa wa Njombe, Yohana Nkwera (54) anadai kukatika miguu katika hali ya kushangaza.
Yohana anasema katika maisha yake amekuwa ni
mwenye hofu kubwa baada ya kukumbwa na tukio hilo la aina yake la
kukatika miguu akiwa usingizini. Anasema hadi sasa haelewi namna hasa
tukio hilo lilivyomtokea, kwani hakuhisi maumivu yoyote .
Anasema tukio hilo la aina yake lilimtokea mwaka
1992, lakini halikuwahi kuandikwa wala kutangazwa, badala yake ni watu
wachache waliokuwa wakilifahamu.
Anasema siku hiyo usiku alikwenda kulala kama ilivyo kawaida, alipoamka asubuhi alikuta miguu yake imekatika.
Kilichomshangaza zaidi ni kwamba hapakuwa na damu
wala jeraha lilionekana. Palionekana pana kovu, kana kwamba alikatika
mguu muda mrefu uliopita.
Anasema mara ya kwanza ulianza kupotea mguu wa
kulia, hiyo ilikuwa ni mwezi Machi, 1992. Kutokana na tukio hilo, ndugu
zangu walifanya jitihada mbalimbali ikiwemo kufanya maombi katika nyumba
mbalimbali za ibada, huku wengine wakienda kwa kuwaona waganga wa jadi.
“Kama binadamu wa kawaida ilichukua muda sana kuamini kilichotokea ndani ya maisha yangu na mguu wangu,” anasema.
Mwezi mmoja baadaye yaani mwezi Aprili mguu wa
kushoto nao ulikatika katika mazingira yaliyo sawa na yale ya
awali.Inaweza kuwa vigumu kuamini lakini ulimwengu ndivyo ulivyo.
Anakumbuka mazingira ya kukatika kwake
yanahusishwa na imani za kishirikina kwa sababu siku chache zilizopita
kabla ya kukumbana na dhahama hiyo aliwahi kukorofisha na mtu katika
vilabu vya pombe za kienyeji anayesadikiwa kufanya tendo hilo.
Baada ya miaka saba kupita Yohana alipelekwa
Hospitali Teule ya Ikonda wilayani Makete kupata huduma za tatizo lake.
Alifanikiwa kupata msaada wa baiskeli ya magurudumu, ambayo aliitumia
kwa miaka mitano.
Kwa sasa baiskeli hiyo haifanyi kazi kutokana na
watu wanaosadikiwa kuwa ni wezi kuiba matairi na vyombo muhimu
vinavyoiwezesha baiskeli hiyo kufanya kazi.
Pamoja na kupewa baiskeli hiyo na wasamaria wema,
Yohana anakiri pia kuchongewa viatu na hospitali hiyo ambavyo
vinamuwezesha angalau kutembea umbali mfupi.
Kutokana na ulemavu huu wa kimiujiza, Yohana anakiri ndoto zake
za maisha hazijatimia mpaka leo na inawezekana zikawa zimepotea kabisa.
Mipango yake
Alipinga mambo mengi yakiwemo kusoma na hata
kufungua miradi ya maendeleo. Sasa ni kama anaona haiwezekani tena kwa
sababu hana uwezo thabiti wa kufanya kazi; ukizingatia ni kijijini
ambako kazi kubwa inayotegemewa kiuchumi ni kilimo cha jembe la mkono.
Ulemavu huo umesababisha ashindwe kuoa, kwani
anasema katika ulimwengu wa sasa ni ngumu kuoana na mtu kama huna uwezo
wa kumhudumia.
Anasema ilikuwa ni ngumu kwa ndugu kuamini
kinachotokea lakini anawashukuru wasamaria wema walioendelea kumhudumia
mpaka pale alipoikubali hali yake na kuanza kuishi katika huo mfumo mpya
wa maisha.
Kwa sasa Yohana anaishi na dada yake mkubwa
aitwaye Lucy Nkwera akimsaidia kwa mahitaji ya kila siku ikiwemo chakula
na huduma za usafi na usalama kwa jumla.
Akisimulia kwa hisia, Yohana anakumbuka jinsi
alivyokuwa katika hali ya uzima wa miguu na kujitegemea, kwamba
anashangaa sana kuona leo amekuwa ni mtu wa kuomba msaada; kwa sasa
msaada wake mkubwa ni dada yake huyo.
Lucy anasema, “Maisha ni magumu sana kwa kuwa anatakiwa kuwa karibu naye, kwani hakuna mwingine wa kumsaidia.”
Mbali na kupata huo ulemavu wa miguu, Yohana anaumwa ugonjwa wa kifafa, ambao nao aliupata baada ya kukatika miguu.
Ugonjwa huu unamfanya kupoteza fahamu mara kwa mara kitendo ambacho ni hatari kwa afya na maisha yake.
Anamshukuru Lucy kwa kuendelea kumhudumia kwa
sababu kwa mazingira ya kawaida ni wachache wenye moyo wa huruma kiasi
hicho, hasa kumhudumia mgonjwa ambaye hatarajii kupona leo hata kesho.
Anashukuru pia ndugu zake kutoka maeneo mengine akisema kuwa nao wamekuwa wakija kumtaka hali na kumletea vyakula.
Anaishukuru Serikali ya Kijiji cha Ludewa anachoishi, kwa kumkumbuka na kumhudumia kwa kadiri wanavyoweza.
Anasema kama Serikali na ndugu wasingekuwa
wanamsaidia, huenda hali yake ingekuwa ngumu zaidi na ilivyo sasa kwani
kwa jumla afya yake ni dhaifu.
Ushauri wake
Yohana anawaomba watu kuachana na tabia za kunyanyapaa walemavu.Anasema baada ya kuwa na ulemavu, kuna marafiki zake walimtenga.
“Inauma sana kuona kumbe wengine ni marafiki wa
wakati wa raha...Ukiwa na matatizo wanakukimbia, hii tabia si nzuri, ni
lazima tuwe na moyo wa kusaidiana wakati wote,” anasema Yohana.
Anaongeza kuwa hata yeye hakupenda kuwa katika
hali ambayo anayo sasa. Ndiyo kusema kwamba yeyote anaweza kupatwa na
lolote kabla ya hajafa, tusinyanyasane.
Na Ayubu Mapunda,Ludewa.
No comments:
Post a Comment