Social Icons

Facebook Twitter LinkedIn Google+

February 26, 2014

WANAWAKE WAPIGWA MARUFUKU KUONEKANA BAR ILI KULINDA SHERIA NA HAKI ZA MTOTO.

 
Wananchi wa Tarafa ya Liganga wilayani Ludewa katika mkoa wa Njombe wameanza kujitungia sheria ndogondogo zitakazowabana wanawake wenye watoto wanaoshinda katika vilabu vya pombe nyakati za usiku ili kuhakikisha haki na sheria za mtoto zinalindwa na kuheshimwa.
 
Hayo yalisemwa jana kwenye ukumbi wa Beach Lugarawa katika kongamano la siku moja lililoandaliwa na shirika lisilokuwa la kiserikali la Lugarawa Development Foundation(LDF) katika mradi wake wa kuhakikisha haki za mtoto zinafahamika na kutekelezwa katika tarafa ya Liganga mradi uliofadhiliwa na The foundation for civil society.
 
Akitoa taarifa na ushuhuda katika kongamano hilo Bi. Annonsiatha mlowe kutoka kijiji cha ilininda alisema kuwa katika kijiji chake tayari sheria hiyo imeshaanza kutumika na baadhi ya wanawake wamekumbwa na sheria hiyo kwa kukamatwa na kuwekwa mahabusu na kutozwa faini ambayo kwa mujibu wa sheria ni fedha hiyo ni sehemu ya mapato ya kijiji.
 
""" hivi karibuni watoto wameanza kupata haki zao kutokana na ofisi ya kijiji cha ilininda kutangaza kuwakamata wanawake wote wanaoonekana katika vilabu vya pombe nyakati za usiku na kuwatoza faini kwani kwa kufanya hivyo wanaume hawataweza kushinda peke yao katika sehemu za starehe hali hiyo itawafanya wawahi kurudi na kupanga mipango na familia zao.’’’ Aliongeza annonsiatha
 
Bi.Annonsiatha alisema baadhi ya watu walishakamatwa na kutozwa faini hivyo mpaka sasa tabia ya wanafunzi watoro imepungua kutokana na wazazi kukaa muda mwingi na familia zao ambapo huwaandalia chakula na kuwasisitiza kuzingatia masomo tofauti na awali.
 
"tuligundua haki za mtoto zilikuwa hazifuatwi kwani watoto wengi walikuwa hawahudhurii masomo kutokana na wazazi wao kutowajali kwa kuwapatia chakula na mahitaji ya shule,lakini tokea sheria hiyo ilivyoanza kutumika tumekuwa tukishuhudia afya za watoto zikiboreka na mahudhurio shuleni yanakwenda vizuri",alisema Bi.Annonsiatha.
 
Akizindua kongamano la kutambua haki za mtoto kwa viongozi wa vijiji wa tarafa ya Liganga afisa maendeleo wa wilaya ya Ludewa Bw.Thomas Kiowi alisema imefika wakati haki za mtoto zinatakiwa kuheshimiwa na kulindwa kwani wazazi wanasahau wajibu zao katika matunzo ya familia.
 
""" shirika la Lugarawa Development Foundation linalofadhiriwa na The Foundation for civil society kupitia mradi wa utoaji elimu ya haki ya mtoto linalengo la kuwakumbusha wazazi wanaoshinda katika vilabu vya pombe za kienyeji nyakati za usiku na kuwaacha watoto wakilala na njaa na kushindwa kuwaendeleza kielimu."" Alisisitiza kiowi
 
Naye afisa tarafa wa Liganga Edward Wayotile alilipongeza shirika hilo kwa kutoa elimu ya haki ya mtoto vijijini kwani umekuwa ukombozi mkubwa kwa watoto hasa kwa wazazi ambao walikuwa wakikwepa majukumu yao na kuwaacha watoto wakilandalanda mitaani na njaa huku wakishindwa kuhudhuria masomo shuleni.
 
Alisema kupitia mradi huo wazazi, watendaji serikalini na wadau mbalimbali wameweza kutambua wajibu zao kwani watoto wamekuwa wakinyimwa haki zao eidha kwa kujua au kutokujua hali ambayo ilipelekea baadhi ya watoto kukimbilia katika miji mikubwa na mashamba ya chai wakitafuta ajira zisizorasmi ili kujinusuru na ugumu wa maisha.
 
Kongamano hilo lilifanyika baada ya shirika hilo kumaliza kutoa semina katika vijiji vya tarafa ya Liganga ambalo liliwakutanisha viongozi wa dini, maafisa watendaji wa vijiji na kata, maafisa tarafa, waandishi wa habari na wadau mbalimbali.
 
mwisho

No comments: