Na Ibrahim Yassin,Rungwe
SERIKALI wilayani Rungwe mkoani Mbeya jana ilisalimu amri kwa
wenyeviti wa serikali za vijiji baada ya wenyeviti hao kutangaza mgomo wa muda
usiojurikana kufanya kazi za serikali katika vijiji vyao wakiishinikiza
serikali kupitia halmashauri hiyo kuwapa stahiki zao.
Hatua hiyo ilifanyika baada ya mkuu wa wilaya ya Rungwe
Chrispin Meela akiwashirikisha
mwenyekiti w a halmashauri
Mwakipiki Mwakasangula pamoja na kamati ya ulinzi na usalama ya wilaya
hiyo kuitisha mkutano na wenyeviti wote wa jimbo la Rungwe magharibi katika
ukumbi wa CCM kwa lengo la kuwataka waendelee kufanya kazi wakati suala lao
linashughurikiwa.
Katika mkutano huo uliokuwa na hisia tofauti huku mkuu wa
wilaya akiwatoa nje ya ukumbi waandishi wa habari kwa madai kuwa mkutano huo
uliwahusu wajumbe pekee ambapo aliwataka
wenyeviti kuwa na subira kwa kuwa suala la posho mbali na kuwa bunge
lilitangaza lakini bado utekelezaji haujaanza na kuwa wanatakiwa wafanye
mikutano kwenye kamati za maendeleo ya kata (KAMAKA) na mihutasari waipeleke
katika ofisi yake ili ianze kufanyiwa kazi
kwenye vikao vyake vya DCC.
“Ni kweli mnafanya kazi katika mazingira magumu ninawaomba
tengueni mgomo,fanyeni kazi huku mkiendelea kufanya mikutano katika vijiji
vyenu,mimi ninaenda Dodoma kikazi nitakaporejea tutafanya mkutano kama huu tena
ili kupeana mrejesho wa wapi mlipofikia huku suala la semina mwenyekiti wa
halmashauri anaendelea kulifanyia kazi” alisema Meela.
Mwenyekiti wa halmashauri hiyo Mwakipiki Mwakasangula kwa upande wake mbali na
kuwapongeza wenyeviti hao kukubali kufanya kazi alisema kuwa hakutegemea kuwa
mkutano huo utafanyika kwa amani kutokana na jazba walizokuwa nazo wenyeviti
hao na kuwa atahakikisha kuwa wataanza kupata semina siku za usoni huku
wakitafuta namna ya kuweza kuwapa posho.
Katibu wa wenyeviti
hao jimbo la Rungwe Magharibi Jonhs Mwakalendile alisema kuwa anapongeza
hatua ya serikali wilayani humo kusikia kilio chao cha kutowapa posho na kuwa
maagizo waliyoyatoa wayatekeleze ili waweze kuendelea kufanya kazi kama zamani
na kuwa wametumika sana katika shughuri za maendeleo bila posho wala semina
hivyo kama suala hilo litafanyiwa kazi hawana budi kuendelea na kazi huku
wakivuta subira ya kupewa stahiki zao.
Alisema kuwa Serikali imeshindwa kutambua jitihada zao na
ndiyo maana imekuwa haiwathamini wakati serikali inaanzia kwenye vijiji lakini
wao wanatoa posho kwa madiwani na maafisa watendaji na wabunge na kuwa katika
bunge la katiba linalotarajiwa kuanza siku za usoni serikali imepanga posho
Tsh,300.000 kwa siku huku wao wakiendelea kupata shida na familia zao na kugeuzwa misukule au mazombi kwa kuzidi kutumikishwa.
“sisi tumekuwa chachu ya maendeleo katika serikali kwa
kuchangisha michango na kusimamia ujenzi wa miradi ya maendeleo lakini serikali
imeshindwa kuthamini jitihada hizo kwa kuwa DC ameahidi kumaliza tatizo hili
katika siku za usoni basi tutaendelea kufanya kazi kwa moyo mmoja huku jicho
letu likiwa kwake kama mambo yatakuwa ni yaleyale basi wataedesha mgomo wa
majimbo yote mawili pamoja na kufanya maandamano makubwa”alisema Mwakalendile.
Wenyeviti hao wa jimbo la Rungwe Magharibi walifanya mgomo
huo wiki iliyopita wakiishinikiza serikali iwape stahiki zao baada ya kusikia
kauli ya Bunge lililoketi Augost 31 mwaka jana kuwa posho za wenyeviti
zinapelekwa kwenye halmashauri za wilaya kila mwaka na wao wakaamua kudai posho
hizo kwa madai kuwa posho zao zinaliwa na wakubwa huku wao wakiendelea kupata
taabu.
Mwisho.
No comments:
Post a Comment