Social Icons

Facebook Twitter LinkedIn Google+

November 13, 2013

WAALIMU WAFANYA KAZI ZAO CHINI YA MITI KWA ZAIDI MIAKA MITATU BAADA YA KUKOSA OFISI.



 Na Ibrahim Yassin,Kyela

BAADHI ya Shule za msingi Wilayani Kyela Mkoani Mbeya zimedaiwa kutelekezwa baada ya kukosa ofisi na kupelekea waalimu kusahihisha madaftari ya wanafunzi chini ya miti huku majengo yaliyojengwa kwa nguvu za wananchi hadi mtambao wa panya Serikali imeshindwa kuyamalizia na kupelekea hali ya ufundishaji kuwa mgumu.

Tanzania Daima ilifanya uchunguzi wa siku tatu na kumalizia katika shule ya msingi Kyangala iliyopo kata ya Talatala Tarafa ya Unyakyusa na kujionea hali hiyo huku viongozi wa Serikali ya Kijiji wakizungumzia shangamoto hizo na kudai kuzitatua.

Mwenyekiti wa Kijiji hicho Fransisi Mwandagane alisema kuwa ni kweli waalimu wamekuwa wakisahihisha kazi za wanafunzi kwenye miti baada ya kukosa ofisi kwa muda wa miaka mitatu na kuwa tayari wamefanya mikutano kadhaa na wananchi ili kujaribu kuondoa changamoto hizo.

Alisema kuwa wamepokea milioni 17 kutoka Serikalini kwa ajili ya ujenzi wa ofisi na wananchi wameanza kuandaa tofari na mchanga ili kukamilisha ujenzi wa ofisi hiyo itakayoondoa tatizo la waalimu kufanyia kazi zao chini ya miti.

Akizungumzia changamoto zingine katika shule hiyo Afisa mtendaji wa Kijiji hicho Ibrahim Mwaipopo alisema kuwa shule hiyo inaupungufu wa waalimu,waalimu waliopo ni sita tu huku matundu ya vyoo yapo sita hali inayopelekea wanafunzi kusubiliana wakati wa kujisaidia huku wengine wakijisaidia vichakani.

Wananchi kwa upande wao walisema kuwa shule hiyo imesahaurika kwa muda mrefu wao wamekuwa wakijitolea michango ya kila namna pindi inapohitajika shuleni hapo lakini pesa toka Serikalini zinachelewa kufika hali inayowakatisha tamaa wao kuendelea kushangia shughuri za maendeleo.

Walisema kuwa katika shule nyingi za msingi wilayani hapa wananchi wamekuwa wakijitolea kujenga majengo kwa mtambao wa panya lakini Serikali imekuwa ikishindwa kuyamalizia na kuwepo kwa mazingira magumu ya kufundisha kwa kuwa wanafunzi wamekuwa wakilundikana katika darasa moja.

Afisa elimu msingi wa Wilaya ya Kyela Cluad Bulle alipofuatwa ofisini kwake ili kulizungumzia sakata hilo hakupatikana na alipopigiwa simu hakupatikana hewani.
Mwisho.

No comments: