MGOGORO mkubwa wa tuhuma za kifisadi zimeibuka Katika
Shule ya Msingi Malungo iliyopo Kijiji Cha Kasala Kata ya Mwaya
wilayani Kyela Mkoani Mbeya baada ya Serikali ya Kijiji hicho
kumtuhumu Mkuu wa shule hiyo Benjamin Said kutumia vibaya Fedha za
Ruzuku,madawati na michango mingine ya wananchi pamoja na matumizi
mabaya ya madaraka.
Tuhuma hizo ziliibuliwa na mmoja wa wajumbe wa kamati ya
shule Kijijini humo na kupelekea kufanyika kwa mkutano ambao
haukufikiwa muhafaka na kupelekea Diwani wa Kata hiyo Aroub Kinana
kumkamata Mwalimu huyo na kumpeleka kwenye kituo kikuu cha polisi
Wilaya ambao walimuweka Lumande na baadaye alikuja kuwekewa dhamana
na viongozi kutoka Ofisi ya Elimu Msingi.
Akizungumza leo na waandishi wa habari Kijijini humo
Mwenyekiti wa Kijiji hicho Seti Mwakasekele alisema kuwa Mwalimu huyo
ni tatizo katika Shule hiyo kwani amekuwa akiyatumia vibaya madaraka
yake na kuwa wao wanamtuhumu kwa ufujaji wa fedha mbalimbali zitokazo
Serikalini pamoja na michango ya wananchi bila kuwashirikisha wenzie.
Mwakasekele alizitaja tuhuma hizo kuwa ni Fedha za
Madawati Tsh,720,000.Ruzuku kutoka Serikalini Tsh,1.888.000,michango
ya watoto wa chekechea Tsh,30.000,Fedha za ukarabati wa shule
Tsh,4,77,600,pamoja na michango mengine ya wananchi,na kuwa matumizi
ya fedha hizo Mwalimu huyo ameshindwa kuzitolea maelezo.
Kutokana na utata huo Halmashauri ya Kijiji iliamua
kuitisha kikao cha dharula na kuwaita waalimu wote mbele ya mratibu
elimu kata Diwani na Afisa mtendaji ambapo walimtaka mwalimu huyo
atoe maelezo kuhusu utata wa fedha hizo na kuwa aliposhindwa kutoa
maelezo waliamua kumpeleka polisi ambapo aliamua kuandika barua ya
kukiri kuwepo na ufujaji huo na kuahidi kuzilipa fedha hizo tarehe
23.09.2013.
Aliongeza kuwa ilipofika siku hiyo hawakuona fedha
yeyote aliyolipa zaidi ya kuletewa lisiti za kufoji ambapo uongozi wa
Kijiji hicho hawakukubaliana na lisiti hizo na ndipo walipoitisha
kikao cha pamojo siku ya tarehe 27.09.2013 kilichowashirikisha
viongozi kutoka Idara ya elimu ikiongozwa na Afisa elimu taaluma
Kassim Mtiro,kamati ya shule na wadau mbalimbali na katika
majadiliano Idara ya elimu iliahidi kumleta mkaguzi ili kujua ukweli
wa jambo hilo.
Afisa mtendaji wa Kijiji hicho Ambele Mwandobo alikiri
kuwepo na tuhuma hizo na kuwa Halmashauri kupitia Idara ya elimu
msingi wameahidi kumleta mkaguzi wa ndani siku ya juma tano ili
afanye ukaguzi wa kubaini tatizo hilo.
Afisa elimu msingi wa Wilaya ya Kyela Cloud Bulle kwa
upande wake mbali na kukiri kuwepo kwa tukio hilo alidai kuwa
wanakijiji ambao ndiyo wenye shule wanamtuhumu Mwalimu huyo na wao
kama Idara watamtuma mkaguzi wa ndani wa Halmashauri ili afanye
uchunguzi ili kubaini ukweli wa tatizo hilo na wao watachukua hatua
stahiki pindi watakapo baini kuwepo na ufujaji huo.
Bulle aliongeza kuwa tatizo kama hilo liliwahi kutokea
katika shule ya msingi Tenende kata hiyo hiyo ya mwaya ambapo
walimtuma mkaguzi ambaye alibaini kuwepo kwa ufujaji na wao kama
Idara ndani ya Halmashauri waliamua kumshusha cheo mwalimu huyo na
kumuamuru alipe fedha zote alizoiba na tayari wanamkata mshahara hadi
pale deni litakapomalizika.
Na
Ibrahim Yassin,Kyela
No comments:
Post a Comment