Social Icons

Facebook Twitter LinkedIn Google+

July 02, 2013

MWENYEKITI WA KIJIJI CHA NINDI KATA YA LUPINGU AWATAKA WANANCHI KUSHIRIKI KIKAMILIFU KATIKA UPIMAJI WA ARDHI.

Wananchi wakiwa katika mkutano wa hadhara ili kunufaika na hati za ardhi za kimila
Afisa mtendaji wa kijiji cha Nindi kata ya Lupingu Bw.Kidulile akihutubia wananchi
Wataalamu wa upimaji wakishauriana jambo
Wataalamu wa upimaji wakifuatilia kikao
                     Wananchi wakifuatilia kikao


WANANCHI wa kijiji cha Nindi kata ya Lupingu wilayani Ludewa katika mkoa wa Njombe wametakiwa kushiriki kikamilifu katika zoezi la upimaji wa Ardhi linalosimamiwa na Halmashauri ya wilaya ili kupata hati za kimila.

Akiongea katika mkutano wa hadhara jana Mwenyekiti wa kijiji cha Nindi Bw.Valentin Henjewele alisema mpango huo wa ulasimishaji ardhi unaofadhiriwa na MKURABITA kupitia Halmashauri ya wilaya ya Ludewa unawataka wananchi wote kushiriki kikamilifu ili kujipatia hati za kimila.

Bw.Henjewele alisema upimaji wa ardhi katika kijiji cha Nindi unatarajia kuanza rasmi tarehe 01 julai na kuisha tarehe 6 julai mwaka huu hivyo kwa yeyote mwenye mashamba katika kijiji hicho hata anaishi vijiji vingine anatakiwa kufika mara moja ili kuweza kupimiwa eneo lake.

Alisema imekuwa ni desturi ya baadhi ya watu kupuuza baadhi ya taarifa wanazopata lakini kwa hili mtu yeyote atakeyeshindwa kushiriki na eneoleke likaachwa,Serikali ya kijiji na halmashauri ya wilaya haitawajibika kwa hilo kwani ni fulsa pekee kwa wananchi wa kijiji cha Nindi ambayo wamebahatika kupata hati za kimila.

“Tumepata upendeleo kwa kijiji chetu kipimiwa Ardhi kwani kuanzia sasa tunaweza kusimama vifua mbele kwa kua tutakuwa na hati za kimila ambazo zitatuwezesha kupata mikopo na hatutaki itokee kuwa mwananchi mwenye eneo nindi ashindwe kupata hati ya kumiliki Ardhi”,alisema Bw.Henjewele.

Nae Afisa mtendaji wa kijiji hicho Bw.Mathayo Kidulile alisema wananchi wamehamasika na upimaji huo wa ardhi kutokana na faida ambazo zitatoakana na hati za ardhi za kimila ambapo wataalamu mbalimbali kutoka halmashauri ya wilaya wamewaelimisha wananchi hao.

Bw.Kidulile alisema uongozi wa kijiji umejipanga vizuri katika kutoa ushirikiano kwa wataalamu hao katika zoezi la upimaji hivyo wananchi wa vitongoji vyote vine wanatakiwa kujitokeza ili kuweza kuonesha mipaka ya maeneo yao.

Alisema kwa wale wanaoishi nje na kijiji hicho lakini wanamiliki maeneo ndani ya kijiji cha Nindi wanatakiwa kurejea mara moja ili kuweza kunufaika na upimaji huo kwani hauna gharama yoyote lakini zoezi hilo likiisha pita atakayehitaji kupimiwa tena itambidi kwenda kwa wataalamu na kupangiwa gharama za upimaji.

Aidha Afisa ardhi mteule wa wilaya ya Ludewa Bw.Joseph Kamonga aliwataka wananchi wa kijiji cha Nindi kutoa ushirikano wa kutosha kwa wataalamu hao ili zoezi hilo la upimaji liweze kukamilika haraka kama lilivyopangwa.

Bw.Kamonga alisisitiza kuwa hakuna gharama ambazo mwananchi anatakiwa kuchangia hivyo kila mwananchi mwenye eneo atatakiwa kujaza fomu kwa majina yake na kupigwa picha yenye sura yake ambayo itaambatana na fomu hiyo yenye taarifa muhimu za mlengwa.

Mwisho.

No comments: