WANAWAKE 70 kutoka
katika vijiji saba vya kata za Lugarawa na Mundindi wilayani Ludewa katika mkoa
wa Njombe wamepata mafunzo ya uelewa juu
ya haki yao ya msingi ya kumiliki ardhi
na kuondokana na mila potofu zinazotokana na mfumo dume nchini.
Mafunzo hayo ya
kuwajengea uwezo yameandaliwa na shirika lisilokuwa la kiserikali la Ludende
Development Assocition (LUDA) na kufadhiriwa na The Foundation Civil Society
(FCS) la jijini Dar es Salaam ambapo Wanawake 70, Maafisa watendaji Kata,
Maafisa Maendeleo ya jamii na Madiwani wa Kata hizo walihudhuria.
Akifungua mafunzo hayo
Bw Labani Shagama ambaye ni Mratibu wa mradi wa haki ya mwanamke kumiliki ardhi
alisema nia na madhumuni ya mradi huu ni kuhakikisha wanawake wanaelewa vyema
haki zao za msingi ili waweze kuzilinda na kuzitetea wao wenyewe.
Bw Shagama alisema
wanawake wengi wamekuwa wakiishi kwa hofu kutokana na kukandamizwa na kutawaliwa na mfumo dume ambao kwa kiasi kikubwa
umewaathiri hata kisaikolojia na kupelekea kunyanyaswa bila sababu ya msingi na
wao kuishia kulalamika kimyakimya wasijue la kufanya.
“” Akaongeza kuwa serikali
imeingia mkataba wa kuchimba madini ya makaa ya mawe ya mchuchuma na chuma cha
Liganga je wanawake wanazijua haki zao za msingi watakazopata kutoka kwa
mwekezaji moja kwa moja na serikali kwa upande mwingine ? “” Shagana aliwauliza
wanawake hao
Washiriki hao wa
Semina walionekana kutokujua lolote kuhusu wawekezaji hao wala taarifa ya nini
kilichomo ndani ya mkataba ulioingiwa kati ya Serikali na wadau hao wa madini
ingawa katika mikutano ya hadhara wanatangaziwa kuwepo kwa wawekezaji hao.
Bw Shagama aliwaambia
washiriki hao kuwa kila mtu anayohaki ya kumiliki mali na mali hiyo yawezakuwa
pesa au mali yoyote ikiwemo ardhi. Kadhalika sheria namba 5 ya ardhi ya mwaka
1999 na namba 2 ya mwaka 2002 zimeweka bayana juu ya umiliki wa ardhi sanjari
na sera ya maendeleo ya mwanamke ya mwaka 2002, iko wazi juu ya wanawake
kumiliki ardhi.
Kwa nyakati tofauti
Wanawake hao walilaumu serikali kutowapelekea elimu hiyo mapema na kwamba kama
wangeipata mafunzo hayo wakiwa wasichana wasingekuwa wanakabiliwa na umaskini
unaotokana na mila potofu zinazowapa wananume nguvu na nafasi ya kuwatumikisha
wanawake kama wanyamakazi hukuwakiambulia ugali tu.
Kwa mujibu wa kifungu
cha 4.2(b) mwanamke anayohaki ya kumiliki ardhi, kupata na kugawa ardhi sawa kwa
masharti yaleyale kama ilivyohaki kwa mwanaume katika kifungu cha 3(2) cha
sera. Ili kuhakikisha mikakati hiyo inatekelezwa sera imeeleza kuwa ugawaji na
upatikanaji wa ardhi utakuwa sawa kwa raia wote.
Mariam Kiswaga pia
alikuwa mmoja wa washiriki aliyeuliza swali kuwa baadhi ya wazazi hasa wazee
watagawaje ardhi kwa watoto wao ambao walishaolewa na tayari pia wana watoto
wao?
Mwezeshaji Bwana Mligo alieleza kuwa kwa wale ambao tayari walishaolewa na
wanafamilia zao mpango huu utakuwa ulishawapita ila wao sasa kama wazazi wanalojukumu la kugawa ardhi bila kujali
jinsia, hivyo watoto wote wagawiwe sawa
Mshiriki mmoja aliyejulikana
kwa jina la Maria N. Mhagama alipopewa nafasi ya kushukuru kwa semina hiyo
katika siku ya tatu ya semina aliomba kuwa shirika la LUDA liangalie namna ya
kusambaza elimu hii kwenye kata za jirani wanazopakana “sisi sasa tumekombolewa
kwani tutamiliki na kumilikisha ardhi” na ikiwezekana waende mbali zaidi ya
kutoa elimu juu ya haki za wajane kwani pamoja na wanawake wakawaida kukabiliwa
na tatizo la umiliki wa ardhi lakini pia ipo shida inayowapata wajane pindi
waume zao wanapokufa.
Sheria ya ardhi ya
kijiji namba 5 ya mwaka 1999,sheria namba 2 ya 2002 na sera ya mwaka 2002,
sheria za kimila hazitatumika wala kupewa uzito kama zitambagua mwanamke,
watoto na wenye ulemavu katika kupata, kumiliki ardhi ya kijiji. Ni lazima
wahusika waeleze kuwa mwanamke anayohaki ya kushiriki katika maamuzi ya kijiji
kwa maana kuwa kila mtu anayohaki ya kupata na kumiliki ardhi kwa ajili ya
matumizi ya msingi.
Kata za Lugarawa na
Mundindi ni Kata ambazo zimo ndani ya migodi ya chuma yaani Liganga na Maganga
Matitu lakini wananchi wa maeneo hayo hawajui nini kinaendelea hadi sasa zaidi
ya kushuhudia magari yakimiminika katika eneo hilo kila kukicha na wala hawajui
haki zao migodi hiyo itakapoanza.
mwisho
Na Bazil Makungu,Ludewa.
No comments:
Post a Comment