Mamlaka ya Mawasiliano (TCRA) imezindua mfumo wa kusajili laini kwa kutumia alama za vidole.
Mfumo huo ujulikanao kama Baiometria utawezesha kupata taarifa sahihi za wateja wa kampuni zote za simu nchini, ilielezwa.
Mfumo
huo umeanza kwa majaribio katika mikoa sita ya Dar es Salaam, Tanga,
Singida, Pwani, Iringa na Zanzibar, ilielezwa zaidi na kila mmmoja
utakuwa na kituo kimoja cha usajili.
Akizungumza
katika uzinduzi huo uliofanyika jana jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi
Mkuu wa TCRA, James Kilaba, alisema hatua hiyo imefikiwa baada ya kuwapo
vitendo vya watumiaji wa huduma kugushi vitambulisho au kutumia
vitambulisho vya watu wengine.
Alisema
ili kukabiliana na changamoto hiyo, TCRA kwa kushirikiana na watoa
huduma za simu za mkononi na Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (Nida)
waliazimia kuanzisha mfumo huo.
"Mfumo
huu ni wa usajili wa laini za simu kwa kutumia Baiometria; yaani mfumo
wa kuchukua taarifa za wahusika kwa njia ya alama za vidole. Kama
tunavyojua kila mtu ana alama pekee za vidole zisizofanana na za mtu
mwingine yeyote duniani," alisema Kilaba.
Alitaja
faida za kutumia mfumo huo kuwa ni kupata takwimu sahihi za watumiaji
wa simu za mkononi na huduma za fedha ambao ni takribani milioni 22, kwa
ajili ya kuweka mipango sawa ya kuendeleza sekta na uchumi wa nchi kwa
ujumla.
Alisema faida nyingine ni kujenga imani kwa watumiaji wa huduma na kudhibiti matumizi ya laini za simu kufanya uhalifu.
Alisema
namba inayosajiliwa kwa majina bandia inaweza kutumika kutapeli au
kutuma ujumbe mfupi wa maneno au simu za matusi na kuudhi.
"Hii
itarahisisha huduma za kuhamia mtandao mmoja kwenda mtandao mwingine wa
simu bila kubadili namba yako, ambayo ilizinduliwa mapema mwaka jana,"
alisema Kilaba.
"Kwa upande wa watoa huduma, usajili utawawezesha kuwajua wateja wao na kuwahudumia kwa ufanisi zaidi."
Vitambulisho
vitakavyotumika kusajili alama za vidole ni cha Taifa, mpiga kura,
leseni ya udereva, kitambulisho cha Mzanzibari Mkazi na hati ya
kusafiria.
No comments:
Post a Comment