Social Icons

Facebook Twitter LinkedIn Google+

September 15, 2014

NAIBU WAZIRI,ZAMBI AWAHAKIKISHIA WAKULIMA WILAYANI LUDEWA UNUNUZI WA MAHINDI.

Naibu Waziri wa kilimo na Chakula Mh.Godfrey Zambi akiongea na wakulima wilayani Ludewa
Mkuu wa wilaya Ludewa akitoa ufafanuzi wa uwingi wa Mahindi wilayani Ludewa kulia kwake na Mh.Zambi akimsikiliza

 Meneja wa NFRA Kanda ya Mkambako Bw.Abdilla Nyangasa akitoa ufafanuzi kuhusiana na tani zitakazo nunuliwa na Serikali
 Naibu waziri wa Kilimo na Chakula Mh.Zambi akikagua mahindi ambayo yameshapimwa
 Mh.Zambi akiwa na ofisa mtendaji wa kata ya Ludewa Bw.Onesmo Haule wakiangalia takataka zilizoko katika mahindi
Mahindi ambayo yamekwisha Pimwa
 Baadhi ya watangazaji wa redio Best Fm akiangalia uwingi wa mahindi
Hapa ndipo panapopimwa Mahindi


Mahindi ya Wakulima yaliyofunikwa kwa kuhofia mvua kuyanyeshea
Baada ya mahindi kuwa mengi mpaka kukosa eneo la kuyahifadhi imebidi kibao hiki kiwekwe


NAIBU waziri wa Kilimo na Chakula Mh.Godfrey Zambi amewahakikishia wakulima wilayani Ludewa kuwa Serikali itayanunua mahindi yao mapema iwezekanavyo kutokana na wakulima hao kutokuwa imani ya kununuliwa mahindi hayo.

Akizungumza na wakulima wa kata ya Ludewa katika kituo mojawapo ya vituo vinne vya ununuzi wa Mahindi wilayani hapa jana Mh.Zambi alisema  Serikali inawathamini sana wakulima kutokana na kutenga bajeti ya zaidi ya shilingi 150 bilioni ambazo zitanunua mahindi nchi nzima.

Imepita miezi miwili hadi hivi sasa wakulima wilayani Ludewa tokea walipomaliza kuyavuna mahindi yao na kuyapeleka katika vituo vya kuuzia lakini hali ilikuwa mbaya sana pale walipokuwa hawana uhakika kama Serikali itayanunua mahindi hayo kwani uvumi mkubwa ulikuwa ni kwamba fedha za kununulia mahindi Serikali imezipeleka kununua mpunga.

Wakulima hao walimweleza Mh.Zambi kuwa wamepata hasara pale ambapo baadhi ya magunia ya mahindi waliyoyafikisha mapema katika vituo vya kuuzia kunyeshewa na mvua na kuharibika vibaya kabla hayajauzwa hali ambayo inawafanya kupoteza mitaji ya kununulia bembejeo za kilimo katika msimu mwingine wa kilimo.

Mh.Zambi aliwataka wananchi kuwa wavumilivu kwani kila jambo linawakati wake kutokana na wakulima wilayani hapa kuilalamikia Serikali kwa kuchelewa kuyanunua mahindi yao kwa muda ambao walizoea kuyauza hivyo yatanunuliwa yote licha ya kuwa mahindi ni mengi kwa mwaka huu.

“Nawapongeza wakulima kwa kuitikia mbango wa kilimo kwanza kwani kwa macho yangu nimeona uwingi wa mahindi mliyoyavuna kwa halii Serikali iko bega kwa bega nanyi kwa kutanunua mahindi yaote hata kama fedha zilizotengwa zitakwisha,mtakopwa na baada ya miezi miwili mtalipwa”,alisema Mh.Zambi.

Mh.Zambi alimsifu Mbunge wa jimbo la Ludewa Deo Filikunjombe kutokana na utendaji wake kwani amekuwa mstari wa mbele kuwatetea wananchi wake na watanzania kwa ujumla na hata ununuzi wa mahindi amekuwa akifuatilia kwa karibu ili kuona mahindi hayo yananunuliwa.

Aidha meneja wa wakala wa manunuzi kanda ya nyanda za juu kusini kituo cha Makambako(NFRA)Bw.Abdilla Nyangasa alisema katika kituo cha kata ya Ludewa zilipangwa kununuliwa tani 3000 lakini kutokana na hali halisi ya uwingi wa Mahindi zimeongezwa tani 2000 na kufikia tani 5000.

Bw.Nyangasa alisema kinachotakiwa kwa wakulima ni kuleta mahindi masafi ili yaweze kuuzika katika mataifa mengine yenye shida ya chakula kwani baadhi ya wakulima wamekuwa wanatabia ya kuuza mahindi machafu wakiamini NFRA watafanya kazi ya kuyasafisha hali ambayo si sahihi.

Alisema wakulima wakitanzania wanapaswa kuanza kujifunza namna ya kuhifadhi chakula ambacho kitaweza kuuzika katika mataifa mengine na si kuishi kwa mazoea kwakufanya hivyo wakulima wanaweza kujiingizia fedha nyingi za kigeni na kuachana na umaskini uliokithiri.

Bw.Nyangasa alisema licha ya Serikali kununua katika kituo hicho tani 5000 pia itaangalia kama wakulima watakua bado wanamahindi basi itaongeza idadi ya tani nyingine kadiri ya itakavyowezekana.

Naye Mkuu wa wilaya Ludewa Bw.Juma Solomon Madaha aliwataka wakulima wanaouza mahindi katika kituo hicho kufuata utaratibu wa waliowahi kufikisha mzigo katika eneo hilo kwa kuwa wakwanza kuyapima mahindi yao.

Kauli hiyo imetoka baada ya baadhi ya wakulima wa hali ya chini kulalamika kwa mkuu huyo kuwa baadhi ya wafanyabiashara wakubwa wamekuwa hawafuati utaratibu kutokana na kujulikana kwa wapimaji wa NFRA hali ambayo inaonesha kuna harufu ya rushwa katika upimaji huo.

Wananchi hao walimpigia simu ya kiganjani kamanda wa TAKUKURU wilaya ya Ludewa na Mkuu wa wilaya hii kuwa makini na jambo hilo kutokana na wafanyabiashara hao wenye zaidi ya magunia 1500 kuwa mstari wa mbele kupima wakati wakulima wadogo wenye magunia 50 kushuka chini wakikesha kituoni hapo wakihofia haki zao kudhurumiwa.

Hata hivyo tayari uongozi wa kijiji umeshaweka kibao kinachoelekeza kusitisha uingizaji wa mahindi kituoni hapo kuokana na nafasi ya kuhifadhia kuwa ndogo ambapo wanunuzi wanashindwa kupata eneo la kuyaweka mahindi ambayo yameshapimwa.

Bw.Madaha aliwaeleza wakulima hao kuwa  uongozi pamoja na uongozi wa kijiji kwa kushirikiana na wafanyakazi wa NFRA wanapanga utaratibu wa nani anatakiwa kuwa wakwanza katika kupima mahindi ili kuepusha migogoro inayoweza kujitokeza katika uuzaji wa mahindi hayo.


Mwisho.

No comments: