Mkuu wa wilaya ya Ludewa Bw.Juma Solomon Madaha akilieleza baraza la Halmashauri namna ya kuyahifadhi mazingira
Uharibifu wa mazingira sio suala geni katika masikio ya jamii
za Kiafrika lakini athari zake ni kubwa tofauti na matarajio ya uharibifu huo
kwani kunabaadhi ya wananchi huharibu mazingira kwa makusudi bila kujua athari
za baadae.
Jamii ya mkoa wa Njombe hasa katika wilaya ya Makete na
Ludewa kumekuwa na uharibifu mkubwa wa mazingira kutokana na kilimo cha kuhama
hama katika vijiji vya pambezoni mwa ziwa nyasa wilayani Ludewa na uandaaji wa
msimu wa kilimo unaolazimu mashamba kuchomwa moto na kuunguza misitu ya asili.
Upitapo wilaya ya Ludewa na Makete sio kitu cha kushangaza
uonapo safu za milima ya Living stone huonekana kuwa na rangi nyeusi hali hiyo
huashiria moto umeshaunguza misitu yote ya asili na kuacha jivu nene juu ya
milima hiyo msimu wa kiangazi.
Pia wakati mwingine milima hiyo ukiwa mbali huonekana kana
kwamba inaukungu mzito lakini ukweli ni kwamba ukungu huo ni moshi mkubwa
kutokana na uchomaji moto uliokithiri katika safu za milima hiyo ambayo
ikitunzwa vizuri ni kivutio kwa watalii wanaokuja kutembelea misitu ya sasili
na viumbe vinavyo patikana katika safu ya milima Livingstone.
Wilaya ya Ludewa ni moja ya wilaya Nchini yenye vivutio vingi
vya utalii hasa misitu ya asili lakini ni wilaya ambayo kwa mwaka 2013
mazingira yake yameharibiwa vibaya kwa kuchomwa moto hali ambayo imesababisha
viumbe kama Nyuki wamekimbia msituni na kukaa katika makazi ya watu ili
kujinusuru.
Mkuu wa wilaya ya Ludewa Bw.Juma Solomon Mdaha hivi karibuni
aliweza kuwaita maafisa watendaji wa vijiji na kuwataka kuwakamata mara moja
watu wanaohusika na uchomaji moto huo holela.
Bw.Madaha anasema sababu kubwa ya misitu ya wilayani kwake
kuharibiwa ni kutokana na msimu wa kilimo kukaribia hivyo wakulima wanaoandaa
mashamba yao kwaajili ya kulima mazao ya mahindi na ngano wamekuwa wakiyandaa
mashamba hayo kwa kuyachoma moto.
Anasema pindi wakulima waandaapo mashamba hayo moto
huwatoroka na kuchoma misitu hali inayosababisha kutokana na sheria kuwabana
baadhi yao hutoroka na kuziacha familia zao katika hali ya upweke kwa kuhofia
kufungwa magerezani.
Alizitaja sababu nyingine ni uwindaji wa wanyama poli na
uchomaji mkaa,kuna wananchi wengine ni wawindaji hivyo kutokana na kuwepo kwa
nyasi ndefu maeneo wanayowindia hulazimika kuzichoma nyasi hizo ili kupata
urahisi wa kuwawinda wanyama hao.
Kuhusiana na suala la uchomaji mkaa mkuu wa wilaya Bw.Juma
Solomon Madaha anasema tatizo hilo lipo kwani wachomaji wa mkaa hupalua mkaa
unaokuwa na moto na kusambaza ili moto huo uzime hali inayosababisha moto huo
kuangukia katika nyasi na kusambaa misituni.
“baadhi ya wananchi bado hawana elimu ya kutosha kuhusu
uhifadhi wa mazingira hivyo nimewaagiza watendaji wa kata na vijiji kutoa elimu
hiyo na kuwachukulia hatua za kisheria wale wote wenye tabia ya kuharibu
mazingira kwa kuchoma moto hovyo misitu isiyo na hatia”,alisema Bw.Madaha.
Anasema hakuna njia rahisi ya kufikisha elimi ya uhifadhi wa
mazingira kwa wananchi walio vijijini zaidi ya vyombo vya habari na watendaji
wa Serikali ambao huishi na wananchi huko vijijini kwa kufanya hivyo hakuna
litakalo shindikana kwani halihalisi ya athari za uharibifu wa mazingira
zimeshaanza kuonekana.
Alizitaja athari hizo ambazo zimeshaanza kuonekana wilaya
Ludewa ni pamoja na kukosekana kwa maji safi na Salama kutokana na miundombinu
ya maji iliyoko katika vyanzo vya maji ambavyo vipo misituni kuharibiwa kwa
moto.
Bw.Madaha alisema wananchi wamekuwa waitupia lawama Serikali
kutokana na ukosefu wa huduma ya maji safi na salama kitu ambacho si kweli
suala kubwa lilalosababisha hali hiyo itokee wilayani Ludewa ni uharibifu wa
mazingira hasa uchomaji moto miundombinu ya maji.
Alisema Serikali wilayani Ludewa inaingia gharama za ununuzi
wa bomba za maji pasipo sababu za msingi kwani wananchi wakielimishwa lawama
Serikalini zitapungua kutokana na tatizo la ukosefu wa maji linavyozidi kukua
siku zinavyoendelea.
Iko haja ya kufanya kampeni kwa kutumia vikundi vya sanaa
huko vijijini ili kuelimisha wananchi umuhimu wa kuyatunza mazingira yao kwa
kutochoma moto hovyo na kuacha tabia ya kulima katika vyanzo vya maji.
Alisisitiza hivi karibuni wananchi wameshindwa kupata maji
safi na salama kwa muda wa wiki mbili sababu kubwa ikiwa ni kuungua kwa
miundimbinu ya maji kutoka katika vyanzo vya maji yanayosambazwa katika mji wa
Ludewa.
Hivyo wananchi ndio wa kulaumiwa na si Serikali kama wengi
wengi wanavyofikiri,kwani upande wa Serikali wanatekeleza wajibu wao lakini
wananchi ndio chanzo kikubwa katika uharibifu wa mazingira kwa kuchoma moto
hovyo hali inayosababisha kuwepo hali ya ukame katika maeneo mazuri ya kilimo.
Chesko Mlelwa mwnanchi wa kijiji cha Amani wilayani Ludewa
akiwa yeye ni mfugaji alisema hali kwa sasa imekuwa mbaya zaidi kwa upande wa
malisho ya Mifugo kwani maeneo ya kuchungia yameteketezwa kwa moto na wakulima.
Bw.Mlelwa alisema imefika wakati wanalazimika kuhama na
kwenda katika maeneo ya mito ambako ndiko kuna vyanzo vya maji kwa wananchi nao
hutegemea huko katika kupata maji kwaajili ya matumizi ya nyumbani.
“Wananchi wamekuwa wakitumia maji pamoja na mifugo yao katika
matumizi ya kila siku hali ambayo inaweza kusababisha binadamu tukaugua
magonjwa ya ajabu kwani awali kulitengwa
maeneo ya mifugo na wanadamu kwa sasa hakuna tena”,alisema Bw.Mlelwa.
Alisema hali hii itazidi kuwa mbaya zaidi kama mvua
zitachelewa kunyesha kwani mazingira yameharibiwa vibaya na uchomaji moto hovyo
unaoashilia kuwepo na jangwa kwa miaka ya baadae wilayani Ludewa.
Mama Lusiana Haule wa kijiji cha Nkomang’ombe wilayani Ludewa
ni mmoja kati ya akina mama wanaopata shida ya upatikanaji wa maji safi na
salama unaosababishwa na uharibifu wa mazingira wilayani humo.
Mama Lusiana alisema hali ya mwaka huu 2013 imekuwa mbaya
zaidi kwani hulazimika kuamka saa nane usiku kwena kisimani kusubiri maji
kutokana na mito kukauka kwa sababu ya uharibifu wa mazingira uliokithiri.
Alisema safari ya kuyatafuta maji huanza kuanzia saa nane
usiku kwa akina mama wa kijiji hicho ambapo hukaa kisimani na kurudi saa kumi
na moja Alufajiri kwani bila kufanya hivyo unaweza usifanye chochote kuwa siku
hiyo.
“Tumekuwa tukikesha visimani na watoto wetu ili kuhakikisha
tunapata maji safi na salama kwani bila kufanya hivyo familia hushinda bila
kula lakin I sababu kubwa ya yote hayo ni uharibifu wa mazingira unaoendelea
siku hadi siku tofauti na zamani kulikuwa na maji maengi kila pahala”,alisema
mama Lusiana.
Kutokana na hali hiyo ya kutumia muda mwingi kutafuta maji
kuna baadhi ya wanafunzi wa shule za msingi huungana na wazazi wao kukesha
visimani na kushindwa kuhudhuria masomo kwani kila siku hurudi nyumbani
asubuhi.
No comments:
Post a Comment