Social Icons

Facebook Twitter LinkedIn Google+

January 30, 2013

FILIKUNJOMBE AUNGANA NA WANAKIJIJI WA MDILIDILI NA MANGALANYENE KATIKA UJENZI WA ZAHANATI.



   

Mbunge wa jimbo la Ludewa katika mkoa wa Njombe Bw.Deo Filikunjombe amewaunga mkono wananchi wa kijiji cha Mdilidili kata ya Lugarawa  na kijiji cha Mangalanyene kata ya madope wilayani Ludewa katika ujenzi wa Zahanati ili kurahisisha huduma za Afya kupatikana kwa urahisi.

Zahanati hizo ambazo zimegharimu zaidi ya shilingi milioni hamsini ziko katika hatua ya mwisho na zimejengwa haraka kutokana na mwamko wa wananchi wa kijiji hicho.

Akikabidhi mifuko 60 ya saruji na tank la kuhifadhia maji katika kijiji cha Mangalanyene Filikunjombe alisema ameguswa na shida za wananchi wake hasa akina mama na watoto kwa kusafiri umbali mrefu ili kufuata huduma ya Afya.

Filikunjombe alisema aliona wananchi hao wanania ya ujenzi kutokana na kujitolea nguvu zao kufyatua tofari hivyo naye akaamua kuwaunga mkono kwa kuajiri mafundi wasimamizi na ununuzi wa vifaa vya viwandani.

Akizungumza na mwandishi wa gazeti hili jana mwenyekiti wa kijiji cha Mdilidili Bw.Ally Ponda alisema zahanati iliyojengwa katika kijiji chake itakuwa ukombozi kwa wananchi kwani awali iliwalazimu kutembea umbali mrefu kufuata huduma ya Afya.

Bw.Ally Ponda alisema Mbunge wao ambaye ni Bw.Filikunjombe amewasaidia kwa kiasi kikubwa katika ujenzi huo kwani wao kama wananchi wamekuwa wakichangia nguvu kazi pamoja na vifaa kama ufyatuaji wa tofari na mchanga.

Alisema Filikunjombe aliweza kumuajiri fundi mkuu na vifaa vipatikanavyo viwandaji hali ambayo iliwarahisishia wananchi hao kwenda haraka katika ujenzi wa zahanati hiyo.

“Tunamshukuru mh.Filikunjombe kwa moyo wake wa upendo kutusaidia ujenzi huu kwani uwali vifo vingi vilikuwa vikitokea kutokana na huduma ya Afya kupatiakana umbali wa kilometa 7 katika hospitari ya misheni ya Lugarawa”,alisema Bw.Ally Ponda.

Aidha alizitaja sababu za ujenzi wa zahanati hiyo ni pamoja na wananchi wanaokwenda katika Hospitari ya Lugarawa kutozwa fedha nyingi wakati wananchi hao bado wako katika hali ya umaskini unaowafanya kushindwa kuchangia huduma za matibabu.

Alisema sababu nyingine ni umbali wa hospitari hiyo hali iliyokuwa ikisababisha akina mama wajawazito kujifungulia njiani na wengine kupoteza maisha kabla ya kufika Hospitari.

Bw.Ally Ponda alisema wananchi wa kijiji cha Mdilidili wana kila sababu ya kumshukuru Filikunjombe kwani awali waliwahi kuahidiwa na wafadhiri katika ujenzi wa zahanati hiyo lakini adhma hiyo haikutekelezwa lakini walivyojaribu kumuomba mbunge wao alikubali na ujenzi ulinza mara moja.

Alisema hiyo ni ishara tosha kuwa Filikunjombe anawajali wananchi wake na hawajutii kumchagua kwani anayoyafanya katika maendeleo ya wilaya ya Ludewa yanaonekana kila vijiji na kata.
Mwisho.



















No comments: