Social Icons

Facebook Twitter LinkedIn Google+

October 23, 2012

KESI INAYOMKABILI MWENYEKITI WA HALMASHAURI YA WILAYA YA LUDEWA BW.KONGO NA WENZAKE YASOGEZWA MBELE



KESI ya kuomba na kupokea manufaa au rushwa inayomkabili mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya ya Ludewa katika mkoa wa njombe Matei Felician Kongo upande wa mashtaka umemaliza ushahidi wake.

Akifunga ushahidi wake jana mbele ya hakimu makazi wa mahakama ya wilaya ya Ludewa Fredrick Lukuna mwendesha mashtaka wa taasisi ya kuzuia na kupambana na rushwa (TAKUKURU) Restuta Kessy akaiambia mahakama kuwa upande wa mashtaka umemaliza ushshidi baada ya kuleta mashahidi wote waliotakiwa katika ushahidi huo.

Katika hali iliyowashangaza wasikilizaji shahidi wa mwisho katika kesi hiyo ambaye anatajwa kuwa rafiki mkubwa wa mshtakiwa Bw Aidani Luoga akaiambia mahakama kuwa machi 12 mwaka huu mshtakiwa alikwenda kwake kuomba namba ya akaunti ya NMB akampa lakini akashangaa siku hiyo majira ya saa 9 mchana akakamatwa na takukuru.

Hata hivyo kabla ya mahakama kutoa amri kama mwenyekiti huyo analo shtaka la kujibu au la wakili wa mshtakiwa Frank Ngafumika akaiomba mahakama isifanye hivyo mpaka upande wa utetezi utakapopewa nakala ya mwenendo wa kesi ili kujipanga kujibu hoja.

Awali ilidaiwa mahakamani hapo kuwa kati ya oktoba mwaka jana na machi mwaka huu mshtakiwa Matei Kongo aliomba rushwa kwa  Samson Mwaipugile mkazi wa Dar es Salaam ili aweze kumpa kwa upendeleo tenda ya ujenzi wa barabara na kusambaza vifaa vya ofisi ikiwemo komputa katika halmashauri ya wilaya ya Ludewa.

Mwenyekiti huyo wa halmashauri ya wilaya ya Ludewa alikamatwa na kufikishwa mahakamani kwa madai kuwa machi 12 mwaka huu alipokea rushwa ya shilingi laki moja (100,000) kwanjia ya benki ya NMB Tawi  la Ludewa kupitia akaunti ya Aidan Luoga.

Kesi hiyo iliahirishwa hadi Novemba 21 mwaka huu itakapokuja kupangwa tarehe ya kuanza kusikiliza upande wa utetezi.

Katika kesi nyingine Afisa mtendaji wa kijiji cha Kipangala katika Kata ya Luilo Ludewa katika mkoa wa Njombe Bw Yohana Jenkin Pili jana alipandishwa kizimbani na taasisi ya kuzuia na kupambana na rushwa (TAKUKURU) kwa kushawishi na kutoa rushwa kwa wananchi ili wasaini vocha hewa za pembejeo.

Pamoja naye waliofikishwa mahakani hapo ni Kilian Kilian Mbawala ambaye ni mwenyekiti wa kamati ya pembejeo ya kijiji cha kipangala na Bw Sebastian Haule ambaye alikuwa wakala wa pembejeo katika kijiji hicho.

Akisoma hati ya mashtaka mbele ya hakimu makazi wa wilaya ya Ludewa Fredrick Lukuna mwendeshs mashtaka wa Takukuru Restuta Kessy akaimbia mahakama kuwa washtakiwa wote kwa pamoja wanakabiliwa makosa 13.

KESSY washtakiwa wote kwa pamoja walitenda makosa hayo mwezi  June mwaka huu ambapo waliwashawishi wananchi kupokea kila mmoja jumla ya shilingi 20,000 kila mmoja ili wasaini vocha hewa kwa faida ya wakala Sebastian Haule, makosa ambayo yanaangukia chini ya kifungu namba 15 cha sheria ya kuzuia na kupambana na rushwa no 11/2007.

Washtakiwa walikana kuhusika na makosa yote yanayowakabili na kdhaminiwa kwa kiasi cha shilingi milioni moja kila mmoja. 

Kesi itakuja kwa kusikilizwa oktoba 21 mwaka huu na upelelezi wa kesi hiyo umekamilika. 

Mwisho.

No comments: