Social Icons

Facebook Twitter LinkedIn Google+

February 25, 2015

SERIKALI ISIMAMIE VYEMA HAKI ZA BINADAMU KWA KUSHIRIKIANA NA SEKTA BINAFSI

   waandishi wa habari kutoka mikoa ya nyanda za juu kusini wakipata mafunzo ya kupinga unyanyasaji wa kijinsia yanayoendeshwa na TAMWA

CHAMA cha Waandishi wa habari Wanawake (TAMWA) kimeishauri serikali  kusimamia vyema haki za binadamu, sambamba na kutoa adhabu kali kwa ajili ya kutatua tatizo la unyanyasaji wa kijinsia nchini.

Vilevile waandishi wa habari nchini wametoa ombi kwa baraza la habari Tanzania (MCT) pamoja na TAMWA kufikiria kuziwezesha klabu za waandishi wa habari za mikoani vyombo vya usafiri ili kusaidia kutumia vyombo vya usafiri wa viongozi (sources).

Hayo yalisemwa jana katika semina ya Tamwa iliyofanyika mjini hapa na kuwashirikisha waandishi wa habari kutoka mikoa ya Iringa, Njombe, Mbeya na Ruvuma.

Akizungumza katika semina hiyo, mwezeshaji wa Tamwa, Wence Mushi alisema serikali inapaswa kuchukua hatua kali ikiwa ni pamoja na kutoa adhabu kali kwa ajili ya kuondokana na tatizo la unyanyasaji wa kijinsia hususani kwa watoto, wanawake na watu wenye ulemavu wa ngozi.

 “Kama sheria za haki za binadamu hazitasimamiwa vizuri na maafisa Ustawi wa Jamii bado ukatili wa aina yoyote utaendelea katika mazingira tunayoishi, hadhi ya wanawake na kuonekana kama ni chombo cha starehe itaendelea kwa sababu haki hazisimamiwi ipasavyo,”alisema Mushi.

Mushi aliwataka wanahabari kuendelea kuibua mambo ya kikatili yanayofanywa na baadhi ya watu hasa kwa watoto, wanawake na walemavu wa ngozi ili kuipa elimu jamii na kushinikiza serikali kuchukua hatua katika ukatili huu.

“Kuna taasisi na mashirika yanayojihusisha na kutetea haki za watoto hivyo ni vyema waandishi kila wanapoona matukio kama hayo yanatokea wakayaibua ili kuyatokomeza kwa kuchukuliwa hatua,”alisema Mushi.

Kwa upande wake mwandishi  Geofrey Nilahi kutoka gazeti la Tanzania Daima, Songea alisema kuwa wanahabari ni chachu ya mabadiliko kama tukiibua mambo ya kikatili yanayofanywa na kushinikiza yafanyiwe mabadiliko hasa katika usimamizi wa sheria na kuchukuliwa hatua kwa wahalifu.

“Wanahabari ni chombo muhimu sana na ili kutokomeza ukatili wa aina yoyote ni lazima kalamu zetu zitumike kukemea mambo yasiyostahili kutedwa na kufuata haki za binadamu ili kuleta usawa katika jamii,” alisema.

Festo Sikagonamo mwakilishi wa ITV Mbeya alisema kuwa endapo wanahabari wakiwezeshwa na  TAMWA kufuatilia habari  juu ya ukatili wa kijinsia pamoja na mauaji ya watu wenye ulemavu hakika mabadiliko yatakuja kupitia kalamu zetu.

Waandishi wa habari walioshiriki mafunzo hayo, waliiomba Tamwa kuwawezesha vyombo vya usafiri vyama vya waandishi wa habari za mikoani (Press Clubs) kwa ajili ya kufuatilia habari katika maeneo ya vijijini ambako wanaamini ndiko habari nyingi zinapopatika.

“Tukiwezeshwa usafiri tunaamini tutaleta habari za kuelimisha jamii, tutaibua mambo mbalimbali na baadaye kuyapatia ufumbuzi kupitia viongozi husika,” alisema George Tarimo mwandishi wa habari Nipashe Iringa.

xxx

No comments: