Social Icons

Facebook Twitter LinkedIn Google+

January 01, 2013

FILIKUNJOMBE APANIA KUJENGA MAWASILIANO MWAMBAO WA ZIWA NYASA.




             
WANANCHI waishio mwambao wa ziwa nyasa katika wilaya ya Ludewa Mkoani Njombe baada ya miaka hamsini ya uhuru sasa wamepata matumaini kwa kupata miundombinu ya mawasiliano ya simu,barabara na usafiri wa majini.

Akizungumza jana katika kijiji cha Nsisi kata mpya ya Lifuma katika tarafa ya mwambao wa ziwa nyasa mbunge wa jimbo la Ludewa Deo Filikunjombe alisema mateso ya wananchi waishio mwambao  yamepatiwa ufumbuzi wa kudumu.

Filikunjombe aliwaambia wananchi kuwa katika kipindi kifupi kijacho atahakikisha mawasiliano ya simu yanaanza ili iwe ukombozi kwa mwambao huo ambapo wamekuwa wakibaki nyuma kimaendeleo kwa kukosa mawasiliano ya simu za mkononi.

Kujengwa kwa miundombinu ya mawasiliano mwambao wa ziwa nyasa kutawasaidia wananchi waishio huko kuwassiliana na ndugu na jamaa wa maeneo mengine pia kutoa taarifa kwa vyombo vya usalama kama kutakuwa na wageni wasiofahamika.

“Ndugu wananchi poleni na mateso mnayoendelea kuyapata ndani ya miaka hamsini ya uhuru mimi mwenzenu niliomba minara mitano ya simu serikalini nikapata mitatu na kati ya hiyo nitahakikisha minara miwili inajengwa mwambao wa ziwa nyasa kati ya kata ya Lupingu na Kilondo ili kuungana na ile ya kyela”,alisema Filikunjombe.

Filikunjombe aliwataka wananchi kuwa na subira kwani wataalamu wa minara watakuja kuangalia ni maeneo yapi mazuri yanayofaa kuijenga minara hiyo ili kupunguza kero zinazowakabili ikiwemo katika Afya ambapo wagonjwa wengi wamekuwa wakipoteza maisha kwa magonjwa ambayo yanaweza kuzuilika kwa kutumia simu za mkononi kuita usafiri.

Akaongeza kuwa mbali ya simu za mkononi filikunjombe aliwataka washiriki katika shughuli za maendeleo ikiwemo kuchimba barabara zinazounganisha kijiji kwa kijiji na kata kwa kata halafu yeye yuko tayari kutoa ushirikiano pamoja na serikali.

Akizungumzia barabara ya Ludewa hadi Lupingu mbunge huyo alisema tayari mkandarasi ameshaanza kazi ya ukarabati kwa kiwango cha changarawe baada ya kuipandisha hadhi na kuwa barabara ya mkoa na kupitia barabara hiyo magari makubwa yatawezo kufika ziwa nyasa.

Hata hivyo mbunge Deo akaondoa hofu iliyotanda miongoni mwa wananchi wake juu uchakavu wa meli ya Mv Songea na Mv Iringa kwa kuwaambia kuwa meli ya Mv Songea inafanya safari zake na Mv Iringa iko mbioni kukarabatiwa ikiwa ni pamoja na utekelezaji wa ahadi ya rais kuhusu ununuzi wa meli mpya ambayo tayari fedha za awali zimeshatolewa.

Awali wakizungumza katika mkutano wa hadhara kwa njia ya risara na kwa nyakati tofauti wananchi walimweleza mbunge wao kuwa wanakerwa sana na ratiba ya meli ya MV songea ambayo inafanya safari zake usiku badala ya mchana ambapo hulazimika kusafiri usiku na kuhatarisha maisha yao.

Akijibu maswali ya wananchi kuhusu meli hiyo kufanya safari zake usiku Filikunjombe aliwaambia kuwa atahakikisha ratiba hiyo inabadilishwa kwa sababu ajali na maafa ya meli kutembea usiku ni kubwa sana ukilinganisha na ajali za mchana.

Kuhusu suala la umeme mbunge alisema anafanya jitihada kuhakikisha umeme unafika katika kata mbili ambazo ni pamoja na Lupingu ukitokea Ludewa mjini na kata ya Makonde umeme huo ukitokea katika kata ya Mawengi unaofadhiriwa na kanisa katoliki.

Kero zingine alizokutana nazo Filikunjombe ni pamoja na wagonjwa, wanawake wajawazito na watoto kutembea umbali na kutumia muda mrefu kufuata huduma za afya katika wilaya jirani ya kyela kwa usafiri hatari wa mitumbwi na maboti yasiyo na uhakika.

Filikunjombe katika ziara yake ya siku tatu mwambao wa ziwa nyasa iliyoanza Disemba 28 hadi 31 mwaka alitoa mifuko mia moja ya saruji katika sekondari ya makonde, na vifaa vya michezo katika kila kijiji ikiwemo ng,ombe mwenye thamani ya shilingi laki tatu kila kata katika wilaya ya Ludewa.

                      mwisho



No comments: