HOSPITALI ya wilaya ya
Ludewa katika Mkoa mpya wa Njombe imo hatarini kupata magonjwa ya mlipuko
kutokana na kukosa chumba cha kisasa cha kuhifadhia maiti zaidi ya miaka kumi
na tano.
Akizungumza na
waandishi wa habari ofisini kwake jana mganga mkuu wa wilaya ya Ludewa
DR.Happines Ndossi alisema kuwa Hospitari hiyo ya wilaya inachumba kimoja tu
cha kuhifadhia maiti chumba ambacho hakiwezi kukabiliana na kasi ya ongezeko la
watu.
DR.Ndossi alisema kumekuwa na shida kubwa ya
uhifadhi maiti kutokana na chuma hicho kutokuwa na majokofu na kuwa na uwezo wa
kuhifadhi maiti mbili tu kutokana na ufinyu wa chumba hicho.
Alisema kuwa kutokana
na wilaya yake kuwa na watu wanaotoka mikoa na nchi jirani kuhamia imekuwa ni
vigumu kuhifadhi maiti zao pindi wanapofariki hali hiyo inawapa shida ndugu na
jamaa wa marehemu na kuwapasa kufanya mipango ya kusafirisha haraka.
“Tuna changamoto kubwa
kwa wananchi wa Ludewa hasa wazee ambao watoto wao wanafanya kazi mikoa mingine
kwani wazee hao wakifariki hatuna uwezo wa kuitunza miili yao ili kuwasubiri
watoto wao kwa mazishi kutokana na ukosefu wa majokofu na vyumba vya kutosha
kuhifadhia maiti”,alisema DR.Ndossi.
DR.Ndossi alisema
kunahatari zaidi kutokana na wilaya hiyo kuwa na wawekezaji wa nchi mbalimbali
katika migodi ya makaa yamawe mchuchuma na chuma liganga kwa kuwa na chumba cha
kuhifadhia maiti kisicho na sifa.
Alisema chumba hicho
kilijengwa tangia wilaya hiyo inaanzishwa kwa takwimu za watu wa kipindi hicho
lakini kwa sasa inahitajika nguvu ya ziada ya kujenga nyumba kubwa ya
kuhifadhia maiti.
Hata hivyo alisema
ofisi yake imeshaandika Bajeti ya ujenzi wa nyumba hiyo na kuiwasilisha ngazi
husika kinachosubiriwa ni utekelezaji tu wa pendekezo hilo.
Aidha alisema licha ya
kutokuwa na chumba cha kuhifadhia maiti pia wilaya yake inakabiliwa na upungufu
mkubwa wa wafanyakazi kwani waliopo hawazidi 50% jambo ambalo ni kero kwa
wananchi.
Alisema kuwa kumekuwa
na vituo vya afya na zahanati zenye mfanyakazi mmoja na nyingine kukosa kabisa
hivyo kushindwa kukidhi mahitaji ya wananchi ambao hujitolea kuzijenga zahanati
hizo wakiwa na lengo la kuhudumiwa ipasavyo.
Ili kupunguza tatizo
hilo DR.Ndossi anaiomba Serikali kuiangalia wilaya hilo kwa jicho la huruma kwa
kuipelekea wafanyakazi kwani wilaya hiyo ni kubwa na ina zahanati 47,vituo vya
afya 6 na Hospitari 3 zisizo na wafanyakazi wakutosha.
No comments:
Post a Comment