WANANCHI katika vijiji
vya Kiyogo kata ya masasi, Ngingama kata ya Lutuhi, Kipingu na Ngerenge katika
kata ya Manda tarafa ya masasi wilayani Ludewa Mkoa wa Njombe wako hatarini kupoteza
maisha kwa kukumbwa na magojwa ya milipuko kutokana na kutumia maji
yanayochafuliwa na wachimbaji madini.
Wakizungumza na mtandao huu jana wananchi hao waliilalamikia serikali pamoja na wawekezaji kwa
kushindwa kutafuta njia mbadala inayoweza kulinda afya zao kutokana na
uchimbaji huo.
Mwenyekiti wa kijiji cha
Kiyogo mzee Ignas Mahundi akaitaka serikali kutoa elimu kwa wananchi kwanza
kuhusu ujio wa wawekezaji katika migodi lakini pia kuweka mikutano kati ya
wananchi na wachimbaji hao ili kuweza kujadili kwa pamoja namna na jinsi ya
kuhifadhi mazingira wakati shughuli za uchimbaji zikiendelea.
“” hatuna maji safi na
salama zaidi ya miaka miwili sasa tunakunywa na kuoga maji machafu yanayotumika
kusafishia madini katika vyanzo mbalimbali vya mto Luhuhu ambao wananchi wa
tarafa ya masasi wanautegemea kwa matumizi ya kila siku. “” alilalamika mzee
LAURANCE MAHUNDI
diwani wa kata ya masasi kwa upande wake akampongeza mwandishi wa gazeti hili
kwa kufanya ziara vijijini kwani ndani ya miaka hamsini ya uhuru wa Tanzania
haijawahi kutokea mwandishi wa habari kukutana na wananchi na kuwauliza
changamoto na matatizo yanayowakabili.
Hata hivyo diwani huyo
akakiri kuwa wananchi wake wanakunywa na kutumia maji yasiyosafi wala salama
yenye tope zinazotokana na shughuli za uchimbaji madini zinazoendelea katika
maeneo ya muhumbi na amani chimbo ambako ndiko kuna vyanzo vya maji.
“” kuanzia sasa mimi
nitahakikisha naishauri halmashauri na serikali kuu kutafuta njia mbadala ya
kuwapatia wananchi maji safi na salama ikiwa ni pamoja na kuchimba visima
virefu au kuwatafutia wachimbaji madini njia nyingine ya kusafisha madini yao na
kuacha kutumia vyanzo vya mto Luhuhu na kama haiwezekani basi wachimbaji hao
waache kuchimba eneo hilo ili kulinda mazingira na afya za wananchi.””
Akashauri Mahundi.
Mzee Mahundi alisema
kuwa miundombinu ya maji safi imefika mpaka kijiji cha Liahagule kilichoko
umbali wa kilomita saba hivyo ni rahisi kuandaa mpango wa kuyafikisha maji hayo
katika vijiji vingine.
Alisema maji yamto
Ruhuhu awali yalikuwa masafi lakini baada ya kuingia wachimbaji wadogo katika
vijiji ambavyo viko katika chanzo cha mto huo imekuwa ni tatizo hata samaki
wameadimika.
Aidha wananchi hao
wameilalamikia Serikali kwa kuwasahau kwa muda mrefu katika huduma ya maji safi
kwani katika kampeni za chaguzi mbalimbali viongozi huahidi bila utekelezaji.
Vijiji hivyo ambavyo
manzari yake yanafaa kwa kilimo cha umwagiliaji vimekuwa ndicho chanzo cha
chakula katika vijiji jirani kutokana na mto huo kuwasaidia katika kilimo kwa
msimu wote katika mwaka.
Aidha Mzee.Mahundi
akaitaka Serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania kuwatendea haki wananchi
wa vijiji hivyo kwa kuwapatia maji safi na salama kama maeneo mengine kwa ndiko
wapiga kura wanakotoka.
CHRISTOPHER NYANDIGA
ni mhandisi wa maji wilaya ya Ludewa kwa upande wake alisema ofisi yake haikuwa
na taarifa kuhusu kuchafuka kwa maji katika mto Luhuhu lakini akaahidi
kufuatilia taarifa hizo na kuchukua maji hayo kuyapeleka kwa mkemia mkuu wa
serikali ili kujua kama yana madhara kwa binadamu na wanyama.
Mwisho.
No comments:
Post a Comment