WANANCHI wa kijiji cha
kimelembe kata ya Mkomang’ombe wilayani Ludewa wamemtimua ofini afisa mtendaji
wa kijiji hicho na kisha kuifunga milango ya ofisi hiyo hadi mkurugenzi wa
halmashauri ya wilaya ya Ludewa atakapompeleka afisa mwingine wa kuchukua
nafasi yake.
Zahama hiyo ya aibu
ilimkuta Bw Ayubu Tematema ambaye alipewa dhamana na serikali ya kukiongoza
kijiji cha Kimelembe kama afisa mtendaji lakini mambo yakawa magumu ambapo
Novemba 18 mwaka huu wananchi walichukua sheria mkononi baada ya kuchoshwa na
tabia za afisa huyo mvivu.
Akizungumza na mtandao huu mwenyekiti wa kijiji hicho Bw James Mtulo alisema kitendo walichokifanya
wananchi wake wamekitenda kwa haki kutokana na mtendaji huyo kujaa kiburi na
kujifanya mungu mtu.
Mwenyekiti
akaorodhesha baadhi ya sababu na tabia mbaya zilizopelekea wananchi kufikia
hatua hiyo kuwa ni pamoja na kutoitisha mikutano ya kusoma mapato na matumizi
katika kijiji hicho.
Mengine ni ulevi,
kiburi, kutafuna michango na uzembe kazini ikiwemo tabia ya kukaidi na kupuuza
maelekezo mbalimbali ya maendeleo kutoka kwenye kamati tendaji ya serikali ya
kijiji.
Aidha mtendaji huyo
amekuwa akiitishwa vikao na kuingia mitini bila kuhudhuria vikao alivyoviitisha
yeye mwenyewe jambo lililochangia kuongeza hasira kwa wananchi wa kijiji chake
na kuamua kufunga ofisi yao.
Kipindi hiki
kilipojaribu kumhoji afisa mtendaji huyo Bw Ayubu Tematema hakuwa tayari
kukanusha wala kukubali badala yake aligeuka bubu na kukimbia camera na vinasa
sauti vya waandishi wa habari.
Diwani wa kata ya
mkomang’ombe Ananias Haule Kajole kwa upande wake alikiambia kipindi hiki kuwa
yeye anaungana na wananchi katika kudumisha dhana ya uwajibikaji na kwamba
mshahara wa mtumishi asiyewajibika siku hizi uko mikononi mwa wananchi wenyewe.
Mkurugenzi wa
halmashauri ya wilaya ya Ludewa Fidelis Lumato alipoulizwa ni hatua gani za
kinidhamu anastahili mtumishi huyo alisema ofisi yake bado haijapata taarifa
hiyo na kwamba anafuatilia kwa maafisa wake kujua kulikoni na kasha atachukua
hatua stahiki.
No comments:
Post a Comment