WANANCHI wa wilaya Ludewa katika mkoa wa Njombe waliieleza
kamati ya tuzo ya rais wasiwasi na kusikitishwa kwao juu ya mikataba ya siri inayowekwa
kati ya Serikali na wawekezaji huku wao wakibaki watazamaji kwa kutojulishwa
kila hatua inayoendelea kwenye migodi ya makaa ya mawe ya Mchuchuma na chuma
cha Liganga.
Hayo yalisemwa jana na wananchi wa kata ya Mundindi mbele ya
mwenyekiti wa kamati ya Tuzo ya Rais ya Huduma za Jamii na uwezeshaji Dr.Rumisha Kimambo katika ziara ya tume hiyo
wilayani Ludewa kwenye migodi ya makaa ya mawe ya mchuchuma na chuma kilichoko
liganga.
Tume hiyo yenye wajumbe saba wakiwemo majaji wastaafu
inafanya ziara nchi nzima ikikukutana na wadau mbalimbali wakiwemo wananchi
wanaoishi katika maeneo ya migodi,wawekezaji na Serikali kwa upande mwingine katika
katika kutekeleza mpango wa mafiga matatu.
Wananchi wa Ludewa pamoja na mambo mengine walitaka kujua ni
lini machimbo yataanza lakini wakataka kujua nini kilichomo kwenye mikataba na
vipi wao watanufaika kupitia wawekezaji wanaotarajia kuchimba migodi ya Makaa
yamawe ya mchuchuma na chuma cha Liganga kama wataweza kutambua fulsa zilizopo
na kuzifanyia kazi.
Akijibu maswali Dr.Kimambo alisema kamati hiyo ya rais ina
kazi ya kutembelea katika migodi mbalimbali nchini ili kuona kama wananchi wa
maeneo ya migodi wananufaika na miradi hiyo ikiwa ni mpango wa Serikali kuona
uwekezaji nchini unaleta faida kwa watanzania.
Alisema dhana ya mafiga matatu ni pana ambapo figa la kwanza
ni mwananchi kuzitambua fulsa zilizopo migodini na kuzitumia,figa la pili ni
mwekezaji kuhakikisha jamii inanufaika na uwekezaji wake ikiwa ni kujenga
miondombinu ya maji,shule,hospitari na mambo mengine na figa la tatu ni
Serikali kusimamia sera ya nchi katika uwekezaji.
“”Serikali ingependa kuona wananshi wake wananufaika na
uwekezaji ulioko nchini na si migogoro inayoendelea kati ya wananchi na
wawekezaji hivyo ikaona ni vyema kuunda chombo kinachofuatilia mambo
yanayopaswa kufanywa na pande zote mbili yenye tija kwa nchi””,alisema
Dr.Kimambo.
Dr.Kimambo alisema kamati hiyo ilianzia kuitembelea migodi ya
kanda ya ziwa na itatembelea nchi nzima ili kuona kwa miaka mitatu wawekezaji
wamefanya kitu gani kwa wananchi hasa katika huduma za jamii na kuondoa
migogoro inayotokea kati ya wananchi na wawekezaji.
Naye Catherine Lyombe
mratibu wa Tuzo ya Rais ya Huduma za Jamii na Uwezeshaji(CSRE) akawatoa
wasiwasi wananchi na kusema Rais Kikwete alizindua tume hiyo ili kuweka uwazi
katika miradi ya wawekezaji kwa kuwa wananchi wanapaswa kutambua faida za miradi
hiyo kwa jamii.
Hata hivyo Catherine akawahakikishia kwamba kupitia tuzo hiyo basi kila mmoja atatimiza
wajibu wake ikiwa ni kuzingatia mikataba aliyoingia na Serikali kama inavyotaka
sera ya nchi kwa wawekezaji waliokwisha anza kazi katika migodi ya kwa zaidi ya
miaka mitatu.
Wananchi wa Ludewa hawawezi kunufaika sasa kwa sababu wawekezaji
bado katika utafiti lakini baada ya kumaliza tafiti zao na kuanza kazi za
uchimbaji ni lazima wazingatie mikataba waliosaini ili kuinufaisha jamii
inayoizunguka migodi ya chuma Liganga na makaa yam awe yaliyoko Mchuchuma.
Ni vema wananchi wa wilaya ya Ludewa waandaliwe ili waweze
kuzitambua fulsa walizonazo na wazifanyie kazi kwani haitapendeza kama hata
mayai, matunda, nyanya, maziwa na nyama
vitaagizwa kutoka katika maeneo mengine wakati wazawa wanao uwezo wa
kuzalisha bidhaa hizo na kuuza migodini.
Akitoa ufafanuzi kuhusiana na kuwaandaa wananchi mkuu wa wilaya ya Ludewa Bw.Juma Madaha
alisema kupitia mradi wa PACA unaoendeshwa na shirika la maendeleo la
Taifa(NDC) wananchi wameanza kuandaliwa ili kuzitambua fulsa zinazowazunguka.
Bw.Madaha alisema mradi huo umeshapita vijijini na unaendelea
kuielimisha jamii jinsi ya kujitambua na kuandaa mipango ya kilimo na ufugaji
utakaowanufaisha wananchi kuuza bidhaa
zao migodini.
Alisema Kupitia MKURAIBITA wilaya Ludewa imeweza kutoa hati za kimila za ardhi
kwa wananchi 95 katika kata ya Mundindi kijiji cha Amani lakini mpango huo wa
kurasimisha ardhi wananchi unaendelea katika vijiji vingine.
Bw.Madaha alisema bado wataalamu wanaendelea kuwashauri
wananchi kutouza maeneo yao ovyo kwa wawekezaji kwani maeneo hayo yataweza
kutumika katika kuzalisha mazao na kuwauzia wawekezaji katika migodi.
Kamati hiyo imeondoka wilayani Ludewa ikielekea mkoa wa Mbeya
katika migodi mingine ili kuielimisha jamii na wawekezaji kutimiza malengo ya
tuzo ya Raisi katika Huduma za jamii na uwezeshaji.
MWISHO.
No comments:
Post a Comment