Mgogoro mkubwa umeibuka wilayani Ludewa kufuatia ugawaji wa
pembejeo za Ruzuku ya kilimo kuto toshereza kwa wakulima tofauti na matarajio
ya wakulima hao ambao wamelima mashamba makubwa na kukosa ruzuku hizo.
Akizungumza katika mkutano wa hazara Afisa mtendaji wa kata
ya Ludewa mjini Bw.Onesmo Haule aliwaambia wananchi kuwa kata ya Ludewa Mjini
zimeletwa vocha 650 zitakazo toshereza kaya 650 wakatika kata hiyo ina kaya
1752 hivyo wananchi wengine hawatapata ruzuku hiyo.
Hapo ndipo hasira ilipoibuka kwa wananchi na kuhoji nani
atapata na nani hatapata ruzuku hiyo na kwa vigezo vipi na kuilaumu Serikali
kwa kuwarubuni kwa sera ya kilimo kwanza wakati sera hiyo haitekelezeki.
Bw.Haule aliwasihi wananchi kutokuwa na jazba kwa tukio hilo
na kuahidi kulifuatilia kwa karibu ili kuona kama utatuzi wa adha hiyo ya
pembejeo za kilimo utawezekana kama wananchi wengi walivyo tarajia.
Aidha Afisa mtendaji huyo aliitupia lawama Serikali kwa
kuwatumia mawakala kusambaza pembejeo hizo badala ya makampuni kama
ilivyotarajiwa na wakulima walio wengi ambapo ingeweza kupunguza bei za
pembejeo hizo.
Bw.Haule alisema Serikali ilipaswa kupeleka fedha za ruzuku
hiyo viwandani na kuyakabidhi makampuni kusambaza kwa wakulima na si mawakala
ambao wamekuwa ni tatizo kila mwaka hali ambayo hudhorotesha sekta ya kilimo
nchini.
“Tumeshangazwa na mfumo huu ambao tumekuwa tukiupigia
kelele kila mwaka kwani hauna tija kwa
wakulima zaidi ya kuwakandamiza wakulima wa hali ya chini kwa kuwaletea vocha
chache ili kuuendeleza umaskini nchini zaidi ya kupunguza”,alisema Bw.Haule.
Akizungumza kwa niaba ya wakulima wengine Bw.Alen Msigwa
alisema Serikali haina nia ya kuwainua wakulima zaidi ya kuwakandamiza na Sera
ya kilimo kwanza haina tija kwa wakulima wa ndani labda wakulima wan je walioko
nchini.
Bw.Msigwa alisema wananchi waliahidiwa kupewa pembejeo za
ruzuku ikiwapo mbolea ya kupandia mazao na mbegu mapema kabla mvua kuanza
kunyesha lakini suala hilo limekuwa kitendawili hasa wilayani Ludewa kwani
mbegu na mbolea hizo zimefika wakati wananchi wameshapanda mazao.
Alisema vocha hizo hazitoshi na kunahatari kusababisha
mgawanyiko wa wananchi kwani watakaopata vocha hizo ndio watakaochangia
shughuri za maendeleo hivyo itawawia vigumu wenyeviti wa mitaa kukusanya
michango ya maendeleo kwa wananchi wasiopata vocha.
“huku ni kusababisha matabaka miongoni mwa jamii kwani ni
kazi ngumu kuwachagua wakulima kuwa nani apate na naniasipate kutokana na hali
hii sasa tunaamini Serikali haina haja ya kutekeleza sera ya kilimo kwanza
kwani dalili tunaziona na kama haiwezekani watoe taarifa na si kuwarubuni
wananchi”,alisema Bw.Msigwa.
Kutokana na hali hiyo Afisa mtendaji wa kata Bw.Haule
aliwataka wenyeviti wa mitaa kukaa na wananchi wa mitaa yao ili kupitisha
majina ya watakaopata pembejeo hizo ingawa zimechelewa na hazitoshelezi
kulingana na uwingi wa wakulima wa zao la mahindi wilayani Ludewa.
Bw.Haule aliusukumia mzigo huo kwa wenyeviti wa mitaa ambao
kwa pamoja walisema wafanyakazi walioajiriwa katika ofisi yoyote hawatapata
ruzuku hiyo wakiwemo wakulima wanaojiweza ili kupunguza mgogoro lakini
waliosomwa kutopata waliapa kutotoa michango ya maendeleo.
MWISHO.
No comments:
Post a Comment