Social Icons

Facebook Twitter LinkedIn Google+

December 05, 2013

ENEO LA UJENZI WA KUMBI ZA MAENDELEO YA VIJANA WILAYANI LUDEWA LATELEKEZWA





Eneo lililotakiwa kujengwa kumbi za maendeleo ya  vijana wilayani Ludewa katika mkoa wa Njombe limetelekezwa tokea mwaka 2003 licha ya kuwa eneo hilo linakibao kinachoonesha kuwa kilizinduliwa na balozi wa Sweden nchini Tanzania Mh.Sten Rylander tarehe 17/05/2003.

Uwekaji wa kibao hicho cha uzinduzi na ujio wa balozi huyo wilayani Ludewa uliratibiwa na shirika lisilo la kiserikali la Student Patnership World Wide(SPW) lakini mpaka sasa hakuna kinachoendelea katika eneo hilo lililopo Ludewa mjini na kusababisha kuwepo msitu.

Kwa mujibu wa maelezo ya mashuhuda katika uzinduzi wa kibao cha ujenzi wa eneo hilo ambao hawakutaka kutajwa majina yao walisema malengo ya ujenzi yalikuwa ni kujenga kumbi tatu kwaajili ya vijana ili kupunguza maambukizi ya virus vya ukimwi.

Walifafanua kuwa mpaka sasa hakuna kinachoendelea kwani pamekuwa ni vichaka ambavyo ni vificho vya waharifu na bado haijulikani fedha za ujenzi wa kumbi hizo ambazo zilidhaminiwa na Ubalozi wa Sweden kama zimeliwa au zilihifadhiwa.

Alipotakiwa kulitolea maelezo suala hilo mkuu wa wilaya ya Ludewa Bw.Juma Solomon Madaha alisema hana taarifa na ujenzi wa kumbi hizo hivyo atalifuatilia na kujua kulikoni na kwanini mpaka sasa kumbi hizo hazijajengwa eneo hilo.

Sina taarifa sahihi ya ujenzi wa kumbi hizo kwani ni inaonesha ni kipindi kirefu kimepita mpaka sasa na hakuna aliyestukia kama kunakibao kilichozinduliwa na Balozi wa Sweden kule vichakani,hivyo nitalifanyia kazi suala hili”,alisema Bw.Madaha.

Bw.Madaha alisema ni jambo jema kama shirika hilo la SPW lilipewa kazi ya kusimamia ujenzi wa kumbi hizo na ubalozi wa Sweden kani vijana wa wilaya ya Ludewa hawana kumbi za kukutania na kujadili mambo yao hasa kufanya mazoenzi ya sanaa mbalimbali.

Aidha viongozi wa shirika hilo walipotafutwa kwa njia ya simu hawakupatikana lakini bado juhudi za kuwatafuta ili waweze kutolea maelezo yanayohusu ujenzi wa kumbi hizo zinaendelea ingawa kuna tetesi kuwa shirika hilo limebadiri jina na ofisi zao ziko mkoani Iringa.

Mwisho.

No comments: