Social Icons

Facebook Twitter LinkedIn Google+

December 15, 2012

MANGULLA AANDALIWA MAPOKEZI MAKUBWA NJOMBE


WAKATI wanachama  wa  chama cha mapinduzi (CCM)  mkoa  wa mpya  wa Njombe  wameandaa mapokezi makubwa  kesho  kwa ajili ya  kumpokea makamu mwenyekiti wa CCM Tanzania bara Philip Mangulla anayerejea  nyumbani toka alipopata kushika nafasi hiyo kubwa ndani ya chama imeelezwa  kuwa nguvu  ya chama cha  Demokrasia na maendeleo (CHADEMA)  mkoa   Njombe imeendelea kuteteleka zaidi .

Sehemu kubwa ya wakazi  wa Njombe  wameanza kuwa na imani  kubwa ya  safu  mpya ya CCM na  kupongeza kuchaguliwa kwa  Mangulla na kupelekea jumla ya wanachama zaidi ya 1000 kutaka  kukabidhiwa kadi  za CCM  na   Mangulla  pindi atakapopokelewa mkoani hapa  .

Duru  za  kisiasa  katika mkoa  wa Njombe  zinadai  kuwa moja  kati ya dalili mbaya  kwa Chadema katika mkoa  wa Njombe ni  matokeo ya uchaguzi  wa serikali za mitaa ambao umefanyika  mara  baada ya wajumbe wa mkutano mkuu  wa CCM kumpitisha kwa  kishindo mwenyekiti  wa CCM Taifa  Rais Dkt Jakaya  Kikwete pamoja na makamu mwenyekiti  huyo Mangulla kwa upande wa bara  na  kupelekea  wanachama  wa  vyama  vyote kuungana  kuchagua viongozi kutoka CCM na Chadema  kujikuta  ikiambulia  vitongoji  3 katika ya 38 huku CUF ikiambulia kitongoji kimoja na  CCM ikivigalagaza vyama  vya upinzani kwa  kupata  vitongoji 34 na  mitaa 25 kati 27 kuchukuliwa na CCM na Chadema kupata  mitaa miwili  pekee.

Hata  hivyo mbali ya  kuteteleka  huko kwa Chadema ambacho kilikuwa  kitamba  kuwa  Njombe ni moja kati ya  ngome  zake kuu bado inaonyesha kubwa  jinamizi  la  viongozi  mbali mbali ndai ya  Chadema  kujiengua na chama  hicho linaendelea kukiandama  zaidi  chama baada ya aliyekuwa mlezi  wa Chama  hicho mikoa ya kusini na aliyekuwa  mgombea ubunge katika  jimbo la Njombe Magharibi Thomas Nyimbo kujiweka kando na Chadema pamoja na makada  wenzake zaidi ya  watatu  na baadhi ya viongozi kuanza kutamani kujiunga na CCM.

Katibu  wa CCM mkoa  wa Njombe Hosea Mpangike  akizungumzia  ujio  wa Mangulla mkoani Njombe  alisema  kuwa ziara  hiyo ni ya kwanza  toka  alipochaguliwa  kuwa makamu mwenyekiti  na kuwa mapokezi makubwa  yameandaliwa  ili  kumpokea  kiongozi huyo ambaye anarejea  nyumbani na  kufanya  shughuli mbali mbali  za chama.

Mpangike  alisema  kuwa  wana CCM na wananchi  wa mkoa  wa Njombe wamekuwa na shauku kubwa ya  kutaka  kumwona kiongozi  wao huyo hasa  ukizingatia  kuwa ni mara ya kwanza  toka alipoondoka nyumbani kuelekea  mjini Dodoma katika  mkutano mkuu  wa Taifa ambao  ndio  ulimchagua  kushika nafasi hiyo.

Alisema  Mangula atapokelewa mida ya saa 6 mchana  katika  mji  wa Makambako ambapo  mbali ya  kuvalishwa  skafu atapata  nafasi ya  kusalimiana na  wananchi mbali mbali ambao wamepanga  kujitokeza  kumpokea pamoja na  kupokea  wanachama  zaidi ya 500 katika mji  huo wa Makambako .

Baada ya kuondoka Makambako mchana  saa 8 atakuwa mjini Njombe katika ofisi ya CCM mkoa ambako atapata nafasi ya  kufungua shina la  wakereketwa ,kusaini  kitabu cha wageni  pamoja na  kupokea taarifa ya chama kabla ya  kusalimiana na wananchi na kupokea  wanachama zaidi ya 500 pia ambao  watakabidhiwa kadi  za  CCM na jioni saa 11 ataondoka Njombe kuelekea kijijini kwake Kinenulo kata ya Imalinyi kwa ajili ya mapumziko ya  sikukuu.

Hata  hivyo Mpangike alimthibitishia  mwandishi  wa habari hizi kuwa hali ya  upepo wa kisiasa katika mkoa  wa Njombe  imegeuka  ghafla na matumaini ya Chadema  kujigamba kuwa  mkoa huo ni ngome yake yamepotea kwa nguvu zaidi baada ya ushahidi  ulioonekana mara baada ya uchaguzi  wa serikali za mitaa kwa  CCM kushinda kwa  kishindo  dhidi ya Chadema  iliyoambilia nafasi  mbili kati ya nafasi 27 kwa uchaguzi  wa vijiji na nafasi  3 kati ya nafasi  38 kwa uchanguzi  wa vitongoji  huku chama cha  wananchi (CUF) wakiambulia nafasi moja  pekee ya kitongoji.

Wakati  huo  huo mbunge  wa  jimbo la Ludewa Deo Filikunjombe amelazimika  kusogeza  mbele  ziara  yake jimboni Ludewa ili kushiriki mapokezi ya makamu mwenyekiti  wa CCM Tanzania  Bara Bw Mangula.

Filikunjombe alisema  kuwa aliona si vema  kuanza  ziara  yake  jimboni kabla ya kumpokea makamu  mwenyekiti  na kuwa ameamua  kuungana na wana CCM wenzake katika mapokezi ya kiongozi  huyo na baada ya  kumpokea Mangula ndipo atakapoelekea  jimboni kwake  Ludewa kwa ajili ya  kuanza  ziara  yake .

Hata  hivyo Filikunjombe  alisema  kuwa safu ya  viongozi  wa sasa ndani ya CCM ni safu ambayo  imekuwa ni tishio kwa  vyama vya upinzani na  kuwa ili CCM kuendelea  kushinda  zaidi katika chaguzi zijazo ni  vema  wana CCM kuendelea  kuipa ushirikiano safu  hiyo ambayo imeonyesha nia ya  kweli ya kuleta mapinduzi ndani ya chama.

No comments: