November 17, 2012
WAETHIOPIA 100 WAKAMATWA WILAYANI LUDEWA
KESI ya kuingia nchini bila kibali inayowakabili wahabeshi 98 kutoka Ethiopia imeshindwa kuendelea katika mahakama ya hakimu mkazi wilaya ya Ludewa katika mkoa wa njombe jana kutokana na wahabeshi hao kukosa mkalimani kuweza kutafsiri lugha yao.
Wahabeshi hao waliokamatwa novemba 13 mwaka huu walikutwa katika milima iliyoko kati ya kijiji cha Ilela na Manda mwambao wa ziwa nyasa ambapo wengine baada ya kuwaona askari walitimua mbio na kutokomea vichakani.
Akiahirisha kesi hiyo Fredrick Lukuna hakimu mkazi katika mahakama ya wilaya ya Ludewa alisema hawezi kuendelea na kesi hiyo mpaka hapo washtakiwa watakapopata mkalimani ili kuweza kutenda haki na washtakiwa kujua shtaka wanalokabiliwa nalo.
Naye mwendesha mashtaka wa polisi inspekta Peter Majengo akaiomba MAHAKAMA isogeze mbele na kupanga tarehe nyingine ya kusikiliza kesi hiyo hadi mkalimani atakapopatikana hata hivyo akasema polisi inaendelea na msako mkali katika mwambao wa ziwa nyasa kufuatia baadhi ya wahamiaji hao haramu kukimbilia porini.
Hata hivyo idadi ya wahabeshi hao imeongezeka leo baada ya wengine wawili kukamatwa na kufanya idadi yao kufikia 100.
Akizungumza na waandishi wa habari hakimu mkazi mfawidhi wa mahakama ya wilaya ya Ludewa Fredrick Lukuna alisema washtakiwa hao walitakiwa kufikishwa mahakamani jana kusomewa mashtaka yao upya lakini imeshindikana kutokana na polisi kukosa usafiri.
“tumeshindwa kuendelea na kesi kutokana na kukosa makalimani wa kuwatafsilia nini kosa lao mpaka wakafikishwa hapa hivyo akipatikana tutaendelea na mashtaka”’alisema hakimu mfawidhi Bw.Lukuna.
Wahabeshi hao kutoka nchini Ethiopia wamekuwa wakitoroka kutokana na ugumu wa maisha hivyo kupita njia za panya ili kufika nchini Afrika Kusini kwa lengo la kujitafutia riziki.
Aidha walirudishwa mahabusu kwa lengo la kutafutiwa mkalimani ili kesi yao iweze kusikilizwa katika mahakama hiyo.
Mwisho.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment