Social Icons

Facebook Twitter LinkedIn Google+

October 26, 2012

SERIKALI WILAYANI LUDEWA YALAUMIWA KWA KUWASAHAU WANANCHI WA KIJIJI CHA KIYOGO


Wananchi wa kijiji cha Kiyogo wilayani Ludewa Katika mkoa wa Njombe wameilalamikia Serikali ya wilaya hiyo kwa kuwasahau kwa muda mrefu hali inayowafanya waishi kama wako kisiwani kutokana na kukosa huduma za msingi ikiwemo maji safi na salama.

Kijiji hicho ambacho tokea enzi za mababu hakijawafi pata maji safi na salama ya bomba wananchi wake wamekuwa wakiugua magonjwa ya matumbo kutokana na kutumia maji yam to Ruhuhu ambayo ni machafu yanayotumika na wachimba madini kuoshea madini maeneo ya wialaya ya Mbinga na kijiji cha Amani.

Akizugumza mwenyekiti wa kijiji hicho Bw.Thomas Magnas alisema anashindwa kuamini kama Serikali haiwatambui wananchi hao kwani kijiji hicho kimesajiriwa kisheria na Serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania lakini wanaishi kama wakimbizi.

Bw.Magnas aliyema ni miaka mingi sasa wananchi wa kijiji hicho wanakunywa maji machafu kuanzia rangi ya maji hayo inatisha kutokana na chanzo cha mto huo kuwepo wachimba madini wanaoyachafua maji hayo hali hiyo imesababisha watu wengi wa kijiji hicho kupoteza maisha kutokana na homa za matumbo.

“Tunaishi kama si Watanzania kutokana na kutokuwa na majisafi na salama kwani hata dhahanati wananchi tumejitolea kuijenga lakini hakuna wafanyakazi hivyo inatupasa kutembea kilimita 15 kufuata huduma hiyi pindi tunapougua”,alisema Bw.Magnas.

Alisema kutokana na magonjwa ya mripuko yanayosababishwa na uchafuzi wa maji hayo huwa inawalazimu kwenda vijiji vya jirani ambavyo ni Lihagule na Masasi wakati mwingine hulazimika kuvuka mto Ruhuhu kwa mitumbwi na kwenda mkoa jirani wa Ruvuma kufuata huduma za Afya.

Katika huduma za Afya wananchi hao waliilalamikia Serikali kwa kutowatendea haki hasa akinamama wajawazito kutokana na umbali wa vituo vya Afya kani baadhi ya akina mama hujifungulia njiani hali hiyo huwafanya wahudumu wa Afya kuwatoza kiasi cha shilingi elfu tano kwa yeyote aliyejifungulia njiani bila kujali umbali wa kijiji hicho mpaka katika vituo hivyo.

Akizungumza kwa uchungu Bi.Gaudesia Jonh alisema wamekuwa wakinyanyaswa kupata huduma za Afya wanapokwenda katika zahanati za vijiji vya jirani hasa nyakati za usiku kwa kuulizwa wanatoka kijiji gani hali hiyo inawakosesha amani kwani wakati wa chaguzi mbalimbali za viongozi huahidiwa huduma za jamii lakini wakishachagua hakuna kinachoendelea.

Bi.Gaudesia alisema hali hiyo ya kutozwa shilingi elfu tano katika vituo vya Afya kwa kosa la kijifungulia njiani si kosa la akina mama hao bali ni kosa la Serikali yao kwani wamejenga zahanati nzuri lakini haina wafanyakazi hali ambayo inawalazimu kutembea kilometa 15 kufuata huduma za Afya ya mama na mototo.

Wananchi hao wlisema bado wanamaswali mengi vichwani mwao kama kweli Tanzania ilipata uhuru mwaka 1961 na kusherekea miaka 50 ya uhuru huo wakati kunawananchi ambao hawana huduma muhumu kama zahanati,maji safi na salama na ujenzi wa shule ya msingi isiyo na sakafu yenye saruji.

Walisema kijiji hicho kinashule ya msingi ambayo ilijengwa na wananchi miaka mingi iliyo pita na kusaidiwa na shirika la Consein kwa kupewa mabati lakini tokea hapo Serikali haikuitupia jicho shule hiyo zaidi ya kuwaleta walimu watatu na wakati mwingine hubaki walimu wawili.

Wanafunzi wa shule ya Msingi Kiyogo bado wanasiriba kwa tope sakafu ya shule yao hali ambayo inawakatisha tama ya kusoma kwani vijiji vya jirani kuna shule nzuri zenye walimu wakutosha lakini kwa kijiji chao hali hiyo imekuwa kitendawili.

Bw.Magnas alisema mpaka sasa wamejenga madarasa manne na ofisi mbili za walimu kwa lengo la kuihamisha shule ya awali kutokana na shule hiyo  kuwa na nyufa kubwa ambazo zinahatarisha usalama wa wanafunzi lakini ni miaka miwili sasa hawana bati za kuezekea majengo hayo waliyoyajenga.

Aidha Bw.Magnas aliiomba Serikali kukitupia jicho kijiji hicho kwa kukisaidia kutokana na kusahaulika kwa miaka mingi ili wananchi waweze kujitambua kuwa wao ni watanzania kama walivyo watanzania wengine na wanastahili kupata huduma za Maji safi na salama,Afya na shule nzuri yenye walimu kama vijiji vingine.

Mwisho


No comments: